Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini, Profesa James Mdoe (katikati mstari wa mbele) akiwa
katika picha ya pamoja ya Mkutano wa MakatibU Wakuu kutoka Nchi
Wanachama wa Kituo cha Afrika cha Sayansi ya Jiolojia na Madini (AMGC).
Wengine katika picha ni wawakilishi kutoka Nchi wanachama pamoja
Makamishna na Wakuu wa Vituo vya Madini.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini, Profesa James Mdoe (katikati) baada ya kufugua kikao
cha Makatibu Wakuu kutoka Nchi Wanachama wakiwa katika Kituo cha Afrika
Sayansi ya Jiolojia na Madini (AMGC). Wengine ni Kamishna wa Madini,
Mhandisi Benjamin Mchwampaka (kushoto) na Assa Mwakilembe (kulia).
Baadhi ya wawakilishi wa Bodi ya
Kituo cha Afrika cha Sayansi ya Jiolojia na Madini (AMGC), wa kwanza
kutoka kulia ni Mwenyekiti wa UNECA, Dkt. Koja Busia, Mwenyekiti wa
Bodi, Masresha Gebreselassie, Mwenyekiti wa AUC, Frank Mugyenyi na
Mkurugenzi Mkuu wa AMGC, Ibrahim Shaddad.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe (anayeongea). Wengine ni washiriki katika kikao hicho.
Mshauri Mwelekezi wa AMGC, Timo
Gawronski akitoa maelezo kwa washiriki wa kikao wakiwa katika maabara
ya uchunguzi wa asili ya madini husika.
…………………..
Tanzania imekuwa Mwenyeji wa Mkutano wa 37 wa Masuala ya Kisera ya Kituo cha Afrika cha Sayansi ya Jiolojia na Madini (African Minerals and Geosciences Center (AMGC) ambao unafanyika jijin Dar es Salaam.
Awali, mkutano huo ulianza kwa
kuwakutanisha Wakurugenzi wa Bodi ya kituo hicho na kufuatiwa na mkutano
wa tarehe 13 Agosti, 2017, uliowashirikisha Makatibu Wakuu kutoka nchi
Wanachama wa kituo husika.
Akizungumza na Vyombo vya Habari
wakati wa Mkutano wa Makatibu Wakuu, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini, Prof. James Mdoe alisema lengo la kukutana ni kufanya
tathmini na kuendeleza yale yaliyopangwa kutekelezwa na nchi wanachama
ikiwemo kupanga mipango ya mwaka ujao na bajeti ya utekelezaji wa
mipango hiyo.
Profesa Mdoe alisema kuwa yapo
mambo ambayo waliyokubaliana katika mkutano wa 36 yakiwemo ujenzi ya
Maabara ya kisasa kwa ajili ya nchi za Maziwa Makuu ambayo itasaidia
katika shughuli za madini ikiwemo za uchunguzi wa madini, kukiwezesha
kituo hicho kufanya shughuli zake vizuri na kusaidia nchi wanachama
katika sekta husika.
Akizungumzia manufaa ya kituo
hicho nchini, alisema kuwa kituo hicho kimekuwa na manufaa makubwa kwa
Tanzania hususan Taasisi za Vyuo Vikuu nchini ambazo zimekuwa
zikikitumia Kituo hicho katika mafunzo mbalimbali.
“Sisi tumepata bahati kubwa ya
kuwepo kwa kituo hiki hapa nchini. Tayari vipo Vyuo na wanafunzi ambao
wamenufaika na uwepo wa kituo hiki. Kwetu sisi ni faida kwa sababu
hatutumii gharama kubwa za kufuata huduma zinazotolewa na kituo hiki
tofauti na nchi nyingine ambazo zipo mbali,” alisema Prof. Mdoe.
Aidha, alisema faida nyingine kwa
nchi wanachama waliolipa ada kamili ni kupata punguzo la asilimia 40 la
kutumia maabara za Kituo hicho.
Akizungumzia malengo ya baadaye ya
kituo hicho, alieleza kuwa ni kukifanya kuwa kituo bora zaidi ikiwemo
kuongeza idadi ya wanachama kutoka nchi nane zilizopo sasa.
Hadi sasa nchi wanachama ni Tanzania, Msumbiji, Sudani Kaskazini, Ethiopia, Uganda, Kenya, Comoro na Angola.
Sambamba na mkutano huo, itafanyika pia sherehe ya kuadhimisha miaka 40 ya kituo husika tangu kuanzishwa kwake.
Tags
Tanzania