Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia baada ya kutunuku vyeti vya
pongezi na shukrani kwa wajumbe wa Kamati Maalumu za Uchunguzi na
Majadiliano kuhusu Rasilimali za madini nchini katika hafla
iliyofanyika Ikulu jijjini Dar es salaam leo Oktoba 23, 2017
……………………………………………………………………….
Jonas Kamaleki- MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewatunuku vyeti wajumbe wa Kamati
za Madini leo Ikulu jijini Dar es Salaam ikiwa ni shukrani kwa kazi ya
kizalendo waliyoifanya.
Akizungumza katika hafla hiyo,
Rais Magufuli amesema kuwa watu hao wamefanya kazi kubwa na ya
kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya watanzania hivyo wanastahili
pongezi.
“Ninashukuru sana kwa kweli mmetengeneza ukurasa wa pekee kwani kazi mliyoifanya ni ya kujitoa sadaka,”alisema Rais Magufuli.
Ameongeza kuwa watanzania wengi
wanaunga mkono juhudi hizi za kulinda raslimali za taifa licha ya kuwepo
watu wachache wanaobeza jitihada hizo na kusema hao inabidi wapuuzwe.
Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa
wameonyesha uzalendo kwa taifa ambalo lina raslimali nyingi lakini
lilikuwa halifaidiki nazo bali zilikuwa zikiwafaidisha watu wachache.
Rais amesema kuwa katika suala la
kutetea na kulinda raslimali za nchi hasa madini, hakuna hata mahakama
ambayo ingeinyima Serikali ya Tanzania ushindi kwani unyonyaji uliokuwa
ukifanyika ulikuwa wa wazi, hivyo ameipongeza Kamati ya majadiliano
chini ya Mwenyekiti wake, Prof. Paramagamba Kabudi.
Amewataka watanzania kuwa na moyo wa kizalendo kwa kujali na kulinda raslimali za nchi bila kuangalia manufaa yao binafsi.
“Ningekuwa na ubinafsi mii
ningekeuwa tajiri sana kwani nimefanya kazi katika Wizara ya Ujenzi kwa
miaka 16, hivyo ningetaka kujitajirisha ningeweza, lakini hivyo vyote
vya nini,” aliuliza Rais Magufuli.
Katika makubaliano kati ya
Tanzania na Barrick Gold Company Limited, mgawanyo wa faida itokanayo na
madini utakuwa 50 kwa 50, jambo ambalo halifanyiki katika nchi yoyote
ya Kiafrika, aliongeza Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Kamati ya majadiliano upande wa Tanzania, Prof. Paramagamba Kabudi
amesema kuwa Rais Magufuli anapaswa kupongezwa kwa msimamo wake katika
suala zima la usimamizi wa raslimali za nchi hasa madini.
Prof. Kabudi amenukuu magazeti ya
Zambia jinsi yalivyompongeza Rais Magufuli kwa hatua hiyo. Amesema kuwa
hakika nabii hakubaliki kwao, nje ya nchi wanampongeza Rais wakati
baadhi ya watanzania wanabeza jitihada hizo.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha
Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba amempongeza Rais magufuli kwa
hatua anazozichukua katika kulinda raslimali za nchi na kuwataka
wapinzani wenzie kumuuunga mkono.
“Mhe. Rais shikilia hapo hapo ili raslimali zetu ziweze kulindwa na kutunufaisha watanzania wote,”alisema Prof. Lipumba.
Baadhi ya waliotunukiwa vyeti
hivyo ni Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai, Prof. Paramagamba Kabudi,
Prof. Abdulkadir Mruma, Prof. Nehemiah Ossolo, James Dotto, Dkt. Yamungu
Kayandabila, Prof. Lwoga, Andrew Massawe, Prof. Rwezaula Ikingula, Dr.
Ambrose Joseph na Prof. Longinus Lutasitara.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na
Mawaziri, Viongozi wa Dini, Viongozi wa vyama vya Siasa, Wakuu wa Vyombo
vya Ulinzi na Usalama,Wanahabari, na wageni wengine ambao walionyesha
kufurahishwa na hatua za Serikali ya Awamu ya Tano katika kulinda
raslimali za nchi.
Tags
MAKINIKIA