Naibu Waziri wa Maji na
Umwagiliaji, Jumaa Aweso akitoa maagizo kwa Mhandisi wa Wilaya ya
Namtumbo, Bakari Mwanyiro (kushoto) na katikati ni Mbunge wa Jimbo la
Namtumbo, Mhandisi Edwin Ngonyani katika mradi wa Rwinga wilayani
Namtumbo, mkoani Ruvuma.
Naibu Waziri wa Maji na
Umwagiliaji, Jumaa Aweso akiwa kwenye mradi wa Milende na Mhandisi wa
Mkoa wa Ruvuma, Jones Kimaro (kushoto) katika Wilaya ya Tunduru, mkoani
Ruvuma.
Naibu Waziri wa Maji na
Umwagiliaji, Jumaa Aweso akikagua moja ya visima viwili vya mradi wa
Matemanga unaotekelezwa katika Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma.
………………..
Wizara ya Maji na Umwagiliaji
imetekeleza agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa kufika Tunduru na
kulipatia ufumbuzi tatizo la maji katika mji huo, alilolitoa siku chache
zilizopita wakati alipofanya ziara ya kikazi katika mkoa wa Ruvuma.
Naibu Waziri wa Maji na
Umwagiliaji, Jumaa Aweso ameweza kufika Namtumbo kwa lengo la kujua
changamoto zinazoikabili wilaya hiyo, ambapo kiwango cha upatikanaji wa
huduma ya maji ni asilimia 21 kwa sasa.
Akizungumza katika ziara yake hiyo
Aweso alisema kuwa kuna haja ya kuchukua hatua za haraka ili kuunusuru
mji huo na hali mbaya iliyonayo, kwa kuipa nguvu miradi inayosuasua na
kuahidi kutuma fedha mara moja ili kufanikisha jambo hilo.
‘‘Nitafanya utaratibu Sh. milioni
300 zinazohitajika zipatikane mwezi ujao, ili utekelezaji miradi
inayosuasua ikamilike mara moja na wananchi waanze kupata maji kama
Waziri Mkuu alivyoagiza kwani fedha ipo na ndio lengo letu kama
wizara,’’ alisema Naibu Waziri.
Pia, Aweso ameagiza wakandarasi
kuacha visingizio na kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa miradi kwa
wakati kulingana na mikataba yao inavyoonyesha na si vinginevyo.
‘‘Umefika wakati wakandarasi
kuacha visingizio ambavyo havina msingi wowote, nawaagiza wakandarasi
wote wanaotekeleza miradi ya maji nchi nzima wakamilishe miradi hiyo kwa
wakati. Kama viwanda vya vifaa mbalimbali vipo nchini, wanunue vifaa
katika viwanda hivyo na si kusingizia kuchelewa kwa vifaa kwa sababu
vinaagizwa kutoka nje ya nchi, wakati hakuna sababu ya kufanya hivyo,’’
alisema Naibu Waziri.
Aidha, Naibu Waziri alitembelea
Wilaya ya Tunduru ambapo hakuridhishwa na hali ya utekelezaji wa miradi
ya maji wilayani humo na kuagiza apate ripoti ndani ya siku tatu
inayoeleza sababu za kusuasua kwa mmoja wa miradi wakati fedha zote za
kutekeleza mradi huo zimeshalipwa na bado haujakamilika.
Tags
MIJI/ UMWAGILIAJI