Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed
Janabi (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania
nchini Saudi Arabia Mhe. Hemedi Mgaza ( wa pili kushoto) pamoja na
Madaktari bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa watoto wa JKCI na Taasisi ya
Little Hearts ya nchini Saudi Arabia. Mhe. Balozi Mgaza alitembelea
Taasisi hiyo leo kwa ajili ya kuangalia maandalizi ya kambi ya upasuaji
wa Moyo kwa watoto na watu wazima inayotarajia kuanza siku ya jumapili
tarehe 10/12/2017.
Balozi
wa Tanzania nchini Saudi Arabia Mhe. Hemedi Mgaza (katikati) akiwa
katika picha ya pamoja na Madaktari bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa
watoto Naiz Majani na Ali Al-Akhfash wa Taasisi ya Little Hearts ya
nchini Saudi Arabia mara baada ya kumaliza ziara yake ya kutembelea JKCI
kwa ajili ya kuangalia maandalizi ya kambi ya upasuaji wa Moyo kwa
watoto na watu wazima inayotarajia kuanza siku ya jumapili tarehe
10/12/2017. Jumla ya wagonjwa 80 wanatarajia kufanyiwa upasuaji wa
kufungua na bila kufungua kifua katika kambi hiyo.
Picha na JKCI
……………
Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Little
Hearts ambao wanafadhiliwa na Taasisi ya Al- Murtada ya nchini Saudi
Arabia wanatarajia kufanya matibabu ya moyo kwa wagonjwa 80 katika
kambi maalum inayotarajia kuanza tarehe 10 – 14/12/2017.
Matibabu
yatakayofanyika katika kambi hiyo ni ya upasuaji wa kufungua kifua na
upasuaji wa bila kufungua kifua (Catheterization) kwa kutumia mtambo wa
Cathlab kwa watoto na watu wazima.
Leo
tarehe 08/12/2017 madaktari bingwa wa Moyo wameanza kufanya uchunguzi
kwa wagonjwa wote watakaofanyiwa upasuaji. Katika kambi hii ya siku
tano tumepanga kufanya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa 30 na upasuaji wa
bila kufungua kifua kwa wagonjwa 50. Upasuaji wa kufungua kifua
utafanyika zaidi kwa watoto na watu wazima watafanyiwa zaidi upasuaji wa
bila kufungua kifua.
Kwa
nama ya kipekee tunaishukuru sana Serikali kupitia Balozi wetu wa nchini
Saudi Arabia Mhe. Hemedi Mgaza kwa kutoa kibali cha kuingia nchini
(Visa) bila malipo kwa wataalamu wetu hawa ambao wamekuja nchini kutoa
matibabu ya moyo bure kwa wagonjwa wetu.
Kama
mnavyofahamu matibabu ya moyo ni ya gharama hivyo basi tunaendelea
kuwahimiza wananchi kujiunga na mfuko wa taifa wa bima ya afya ambao
utawasaidia kulipa gharama za matibabu pindi watakapougua na kuhitaji
kupata matibabu.
Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano na Masoko
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
08/12/2017
Tags
AFYA