
Kijana mmoja ambaye
amefahamika kwa jina la Mohamedy Msangi (28) mkazi wa Kilakala Manispaa
ya Morogoro anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kughushi
nyaraka na kujipatia mkopo wa milioni 15 katika taasisi ya mfuko wa Rais
Kanda ya Morogoro.
Kamanda wa polisi mkoa wa
Morogoro Ulrich Matei amethibitisha kutokea kwa jambo hilo na kusema
kuwa jeshi la polisi lilipata taarifa na askari walifuatilia na
kumkamata mtuhumiwa huyo ambapo baada ya kuhojiwa alikiri kufanya kosa
hilo kwa kuomba mkopo katika taasisi hiyo inayojihusisha na utoaji wa
mikopo kwa vikundi vya wanawake na vijana.
Matei amedai kuwa kijana
huyo alipoomba mkopo huo aliorodhesha majina ya vijana wengine wanne
akijifanya kuwa vijana hao wamejiunga kwenye kikundi hicho kisha
kupatiwa mkopo huku hao vijana aliowaorodhesha wakiwa hana taarifa
yoyote.
Mbali na hilo Kamanda
Matei alitoa rai kwa wananchi wa Morogoro na kuwataka wananchi kuacha
wizi "Tuache huu wizi kwa kutumia vyombo vinavyotoa mikopo kwani mikopo
hii imewekwa kwa ajili ya kuwasaidia watu wa chini na hilo ndiyo lengo
la Serikali kuwaondolea watu umasikini ili waweze kufungua viwanda
vidogo vidogo na kujipatia kipato, lakini wapo watu wanatumia vibaya
vikundi hivi" alisema Matei
Tags
UTAPELI