Dauda amesema, kabla ya kuijunga na vilabu vikubwa ambavyo vinapresha ni muhimu kujua sifa za klabu husika na wachezaji utakaokutana nao kwenye nafasi unayocheza, pia ni muhimu kuwa na mtu sahihi wa kukushauri mambo mbalimbali.
“Klabu kama Yanga ambayo ina presha kubwa ya mashabiki wanaotaka matokeo ya ushindi, makocha pia wana presha wanahitaji timu zao zipate matokeo ya ushindi, hakuna muda wa uvumilivu. Timu inaweza ikashinda mechi tano mfululizo lakini bado mechi ya sita ukawa na presha ya kushinda, kifupi hayo ndio maisha ya vilabu hivi viwili na vilabu vingine vikubwa duniani.”
“Sasa wachezaji ambao wanapata nafasi adhimu ya kuvitumikia hivi vilabu wanakuwa wamejiandaaje kisaikolojia? Wachezaji wa kigeni kama Kamusoko, Ngoma, Niyonzima, Kotei, wanakuja wakiwa wanajua watakutana na ushindani na wanatakiwa kuonesha kile ambacho watu wanasubiri kukiona toka kwao.”
“Kwa kijana kama Juma Mahadhi ambaye ametoka Coastal Union ya Tanga kwanza yeye ndio alikuwa star wa timu na Danny Lyanga. Lyanga akasajiliwa Simba, Mahadhi akaenda Yanga, kumbuka kwamba alivyokuwa Coastal Union yeye alikuwa star sasa anavyoingia Yanga anakuja na u-star wake, akija Yanga anakutana na ma-star waliopo na yeye anatakiwa kuingia ili kushindania namba.”
“Ukifuatilia wachezaji wengi sana mtu kama Paul Nonga anatoka Mbeya City na Mwadui akiwa super star anavyoingia kwenye safu ya ushambuliaji ya Yanga anakutana na ushindani wa maana kutoka kwa Ngoma na Tambwe anaamua kurudi zake Mwadui ambako anafunga magoli kila kukicha.”
“Unapokwenda Yanga unatakiwa kujua ni klabu yenye sifa za aina gani, nafasi unayocheza kuna wachezaji wa aina gani, kwa hiyo unapokwenda kuwa mtulivu na mvumilivu, msikilize mwalimu na ujitoe mazoezini kwa sababu moja ya njia ya kumshawishi mwalimu kukupa nafasi sio kumpa ‘shikamoo’ kila mnapokutana.”
“Unaweza ukawahi kila siku mazoezini lakini usimvutie kwa hiyo komaa ili umvutie mwalimu, jua miiko, wahi mapema mazoezini mwalimu akukute. Jitoe mazoezini kwa asilimia 100, wachezaji wengi wa kitanzania mazoezini huwa wanafanya mazoezi halafu kwenye mechi wanataka wacheze mechi lakini kumbe ni kinyume. Mazoezini ndio mahali ambapo unatakiwa ucheze mechi kwa maana ya kujitoa kwa asilimia zote ili ukiwa kwenye mechi ufanye kilekile unachokifanya mazoezini.”
“Sasa wachezaji wetu wakija huku juu, TV, magazeti, radio, unakuwa unazungumzwa wewe, unaanza kupokea simu nyingi kuliko ilivyokuwa mwanzo sasa una mtu wa kukushauri vizuri? Kwa mfano wakati wa mazoezi simu weka silent iache sehemu ukitoka mazoezini pumzika achana na simu na ikiwezekana badili kabina ‘line’ uliyokuwa unaitumia awali kwa sababu kuna watu wengi ambao wanaifahamu.”
“Jali sana muda wa kupumzika, achana na mambo ya mitandao ya kijamii inapofika wakati wa kupumzika, jipangie kwamba ikifika muda fulani lazima uwe umelala ili asubuhi uwahi mazoezini. Ukilala saa nane usiku kwa sababu ya kufatilia mambo ya mitandaoni na kuchati ukiamka unakuwa umechoka huwezi kuwa sawa mazoezini matokeo yake unaanza kulalamika unapigwa misumari.”
Tags
Shaffih Dauda