
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla, amesema hatajibu maombi yoyote yaliyowasilishwa ofisini kwake kutoka kwa wakuu wa mikoa, halmashauri pamoja na wakuu wa wilaya ya kufuta maeneo ya hifadhi, ili maeneo hayo yatumike kwa ajili ya matumizi mengine.
Amesema maeneo hayo yalitengwa kisheria na yana umuhimu mkubwa kiuchumi na kijamii, hivyo lazima yaendelee kuhifadhiwa kwa ajili ya faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Amesema katika kipindi cha uwaziri wake hatajibu ombi lolote lile linalohusu kubadili matumizi ya maeneo hayo kwa vile kuwa na misitu sehemu za mijini ni sehemu ya maendeleo.
Aliyasema hayo jana mjini Iringa alipokuwa akizungumza kwa mara ya kwanza na kamati ya kitaifa ya ushauri wa misitu iliyokutana kwa ajili ya kufanya kikao chake cha tatu tangu ilipoundwa mwaka jana, ikiwa pamoja na kutembelea msitu wa Hifadhi wa Kihesa Kilolo uliombwa na uongozi wa mkoa kufutwa, ili upate kutumika kwa kuweka miundombinu mipya ya mji wa kitalii.
Katika kikao hicho ambacho Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alishiriki, Waziri Kigwangallah alimuomba mkuu huyo awafikishie ujumbe wakuu wa mikoa wengine ambao walituma na wanaotarajia kutuma maombi ya namna hiyo kuwa yeye hatakaa hayajibu hadi pale tu yule aliyemteua ampe maelekezo na si vinginevyo.
Alisema halmashauri nyingi nchini kila zikiona maeneo ya hifadhi zimekuwa zikifikiria kubadili matumizi ya maeneo hayo, ili yatumike kwa shughuli zingine za maendeleo kama vile kupima viwanja ili kuwauzia wananchi kwa lengo la kukusanya mapato.
"Ofisini kwangu kuna maombi mengi mno ambayo hata sielewi nianze na lipi na niache lipi, nasema sitajibu ombi lolote lile," alisisitiza Kigwangalla.
Waziri Kigwangallah baada ya kuzungumza na kamati hiyo, alitembelea eneo la hifadhi ya msitu huo huku akiwa ameongoza na kamati hiyo pamoja na Uongozi wa Mkoa wa huo.
Katika ziara hiyo, Kigwagwalla aliwashukia viongozi wa Halmashauri kwa kuanzisha dampo katika eneo hilo, huku kamati ikijionea magari matatu ya taka yakiendelea kumwaga uchafu kwenye eneo hilo jambo ambalo ni kinyume cha sheria za uhifadhi.
Tags
Dk Kigwangalla