Wakati wanawake wakisherekea siku ya wanawake duniani,Nesi
aliyejulikana kwa jina moja la Hilda akiendelea kuhudumia wagonjwa
katika kituo cha afya cha Bunambiyu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga
amejikuta katika wakati mgumu baada ya kushambuliwa kwa kuchapwa vibao
na diwani wa kata ya Bunambiyu Richard Sangi Sangi (CCM).
Inaelezwa kuwa chanzo cha tukio hilo lililotokea leo Alhamis Machi
8,2018 majira ya saa tatu na nusu asubuhi, ni diwani huyo kumtuhumu nesi
huyo kuwa hahudumii wagonjwa vizuri na kumtaka aondoke kituoni na
alipogoma ndipo diwani alipoamua kumshambulia nesi huyo mbele ya
wagonjwa.
Malunde1 blog imeambiwa kuwa diwani huyo alipigiwa simu na wananchi
wakimwelezea kuwa mgonjwa wao aliyelazwa katika kituo hicho cha afya
kwa zaidi ya wiki moja hapatiwi huduma vizuri na ndipo diwani huyo
alipoomba kuongea kwa simu na nesi aliyepo zamu,nesi akamsihi diwani
afike ofisini/kituoni na alipofika akaanza kumshambulia nesi huyo.
“Huyu diwani amekuwa kama rais,wananchi wanapeleka
malalamiko yote kwake,alipigiwa simu kuwa mgonjwa wao hapatiwi huduma
vizuri hali inayosababisha aendelee kulazwa”,kilieleza chanzo cha habari cha Malunde1 blog.
Hata hivyo habari zaidi zinasema,wakati nesi Hilda akiendelea
kuhudumia wagonjwa,ghafla nesi mwingine ambaye hakuwa zamu aliingia
katika wodi ya wagonjwa na kuwaambia ndugu wa mgonjwa huyo kuwa ndugu
yao ana upungufu wa damu hivyo anatakiwa kupewa rufaa kwenda hospitali
ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga.
“Kutokana na hali hiyo ndipo ndugu wa mgonjwa wakaamua
kumpigia simu diwani na kutaka kuongea kwa simu na nesi wa zamu,nesi
akaomba diwani afike ofisini,alipofika ndipo akaanza kuonesha ubabe kwa
kumshambulia nesi ambaye alikuwa zamu na alikuwa anasimamia kituo cha
afya kutokana na mganga mkuu wa kituo kutokuwepo kazini”,kilieleza chanzo chetu.
Taarifa ambazo mtandao huu umezipata ni kwamba tayari nesi huyo
ameelekea kituo cha polisi kutokana na tukio hilo la kushambuliwa na
kudhalilishwa na diwani huyo.
Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kishapu,Josephine Matiro amesema tayari amepokea taarifa za tukio hilo na anazifanyia kazi.
Tags
madiwani