MAKALA SIMULIZI- DARASA LA CHANETA

DARASA
LA CHANETA
Adeladius Makwega-DODOMA
Mei 20, 2022 niliingia
Bungeni nikiambatana na viongozi wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambao
waliwapokea viongozi wa CHANETA-Chama Cha Mpira wa Netiboli Nchini waliokuwa
wageni wa Naibu Waziri Pauline Gekul.
Mara zote ninapokuwa na mtu
mgeni lazima kuna jambo huwa najifunza kwake, je CHANETA walinipa darasa la
nini?
Darasa lao lilikuwa la
Mchezo wa Netiboli tu ambalo lilijikita katika masomo makubwa mawili. Kwa kuwa
mimi ni mkarimu ngoja nikugawie masomo hayo.
Somo la kwanza lilikuwa juu
ya jina halisi la mchezo wa NETIBOLI, niliambiwa kuwa jina lao na siyo mpira wa
pete kama linavyotumika na baadhi ya wadau bali mchezo wa NETIBOLI.
“Mchezo wetu ni kweli unayo
hiyo pete, una nyavu, unao mlingoni. Pete inayotajwa ina kipenyo cha milimita kati
ya 380-450, mlingoni unakuwa na urefu wa mita 3.55 ambapo nusu mita huwa
inazama ardhini wakati inachimbiwa na mlingoni ukiwa uwanjani una urefu wa mita
3.05.”
Haya aliniuma sikio Dkt
Devotha Marwa ambaye ndiye mwenyekiti wa CHANETA.
Kiongozi huyo wa chama cha
michezo huu nchini alisema kuwa urefu wa uwanja wa mpira wa netiboli ni mita
30.50 na upana wake ni mita 15.25 ndiyo kusema Mita 30.50 kwa Mita 15.25. Unaposema
mpira wa pete ni kuviweka kando vifaa vyote vinavyotumika kuukamilisha mchezo
huo kuchezwa.
“Uwanja wa Netiboli
unatazama kati ya Kaskazini na Kusini ili kutoa nafasi ya jua linapochomoza na
kuzama kutoelemea wachezaji wa upande mmoja. Kila timu inaonja joto ya jiwe la
jua uwanjani. Kama uwanja huo ungekuwa unatazama Mashariki na Magharibi hali hiyo
ingependelea timu moja na kuumiza timu nyingine kwa miale ya jua.”
Dkt.Marwa alidai kama uwanja
wa Netiboli ukiwekwa vizuri unaweza kutumiwa hata kwa michezo mingine kama vile
mpira wa wavu kwa kuwa vipimo vyake havitafautiani sana.
“Tunawahimiza Watanzania
wengi kuupenda na kuucheza mchezo huo kwani kiwanja kinaweza kuchezwa hata
kikiwa na majani, mchanga na sakafu. Gharama za vifaa vyote tangu pete,
mlingoni, mpira, wavu na kuweka sawa uwanja ni shilingi 200,000/ Je kwanini
watoto wetu hawachezi mchezo huo?” Aliuliza.
Hayo yote yalitoka katika
somo la kwanza la CHANETA.
Somo la pili lilijikita katika
vionjo vya ndimi zangu zilipowatazama viongozi hawa, walikuwa ni watu wa
mazoezi kweli kweli huku wakiwa na siha zilizojengeka vizuri sana. Katika
michezo mambo yanapendeza mno kama viongozi wa vyama vya michezo waliwahi
kuucheza mchezo huo, mathalani TFF na BMT enzi za Leodga Tenga katika soka.
Dada zangu watatu Shy-Rose
Bhanji, Beth Mkwasa na binti mmoja ambaye jina lake japokuwa nililihusudu
kulijua lakini sikujaliwa kulipata, wao walikuwa na miili ya wastani huku ikiwa
imara sana, nikasema kweli Netiboli imepata uongozi.
Nilipouliza juu ya wao
kuucheza mchezo huo nilijibiwa kuwa wote ni mabingwa wa kuucheza na kuufundisha
mchezo huo. Shy-Rose Bhanji niliambiwa anacheza CENTER(C) Beth Mkwasa GOAL
KEEPER (GK) naye Dkt. Devotha Marwa WING DEFENCE (WD) binti niliyetamani
kulifahamu jina lake lakini wapi yeye niliambiwa anacheza GOAL SHOOTER (GS)
hizo zote habari ndogo, habari kubwa ipo kwa WINGER ATTACK (WA)-Rose Mkisi,
GOAL DEFENCE (DF)–Hilder Mwakatobe na GOAL ATTACK (GA)-Mary Chalamila.
Narudi kulisema kwa Rose
Mkisi na Mary Chalamila maana habari zao zilikuwa makini mno katika kuucheza mchezo huo. Kweli Netiboli
kumekucha, lakini nisiumalize uhondo huo.
Wakiwa uwanjani watajipanga
hivi GK-GS,WA-WD,GA-GD,C-C,GA-GD,WD-WA na GS-GK. Ndiyo kusema Mkwasa, Mkisi,
Chalamila, Bhanji, Dkt Marwa, na yule binti nisiyemfahamu jina atacheza–Goal Shooter.
Huku Shukuru Kiwege na Kilongozi Ray wakiisimamia timu hiyo.
Kwa maelezo ya Naibu Waziri
wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul ni kuwa timu bora za Netiboli zipo
nyingi sana hasa hasa timu ya TAMISEMI. Kwa kauli hiyo ya natamani uongozi wa
CHANETA ucheze mechi ya kirafiki na timu ya TAMISEMI.
Mie mwanakwetu nitakuwa
kando kuukodolea macho mpambano huo, naisubiri siku hiyo kwa hamu kubwa. Nyie si mnapenda soka? Endeleeni na habari za
Simba na Yanga za kupandishana presha mie
naendele na Netiboli yangu,
Huku timu zetu zinachanja
mbuga kimataifa kila uchao.
Kabla ya mpambano huo
kufanyika naomba nitoe rai kwa timu ya Netiboli ya TAMISEMI chonde chonde msiniumizie
Dkt Devotha Marwa katika mechi hiyo.
Hadi hapo masomo yangu
mawili ya darasa la CHANETA yamekwisha.
Maswali yanakaribishwa