DKT MABULA AZINDUA KAMATI YA KUPINGA UKATILI NA UNYANYASAJI WA KIJINSIA YA UWT ILEMELA
Kamati ya kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ya jumuiya ya wanawake wa CCM wilaya ya Ilemela imezinduliwa leo na mbunge wa jimbo hilo Mhe Dkt Angeline Mabula ikiwa ni utekelezaji wa agizo la mwenyekiti wa chama hicho ngazi ya taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hasan na kuungwa mkono na mwenyekiti wa UWT taifa Ndugu Mary Chatanda
Akizungumza
na wajumbe wa kikao cha baraza kuu la UWT wilaya ya Ilemela katika ofisi
za CCM za wilaya hiyo zilizopo kata ya Buswelu, Mgeni rasmi na mbunge wa jimbo
la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amewataka wajumbe wa kamati hizo kwenda
kutekeleza wajibu wao kikamilifu kwa kuhakikisha wanafichua vitendo vyote vya
kikatili na kuchukua hatua kali dhidi ya wanaofanya vitendo hivyo ili kuunga
mkono maono ya Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt Samia Suluhu Hasan alipozitaka
jumuiya za CCM kupambana na vitendo vya kikatili na unyanyasaji katika jamii
‘.. Mhe Rais Dkt Samia alielekeza jumuiya zipambane na ukatili na
unyanyasaji wa kijinsia, Lakini hakuna aliyechukua hatua mpaka alipokuja mwenyekiti
wa UWT taifa Ndugu Mary Chatanda, Amezunguka nchi nzima mikoa yote kukemea hili
na yote kwa sababu tuna Rais kinara anaepinga vitendo vya kikatili na
unyanyasaji na nyinyi wenyewe ni mashahidi wa hili ..’ Alisema
Aidha Dkt Mabula mbali na kuwataka wajumbe hao kuyasema mazuri
yaliyofanya na Serikali amempongeza Rais Mhe Dkt Samia kwa kuanzisha wizara
itakayosimamia maendeleo ya jamii na jinsia kwani itasaidia kupunguza na kuzuia
vitendo vya kikatili kwa kuwa itakuwa ikisimamia masuala hayo moja kwa moja
tofauti na hapo awali ambapo wizara moja ilikuwa na mambo mengi kiasi cha
kutoyapa sana kipaumbele mapambano dhidi ya ukatili na unyanyasaji
Kwa upande wake mjumbe wa kikao hicho ambae pia ni katibu wa CCM
wilaya ya Ilemela Ndugu Hasan Milanga amekemea vitendo vya baadhi ya viongozi
kushiriki vikao vya kampeni kabla ya wakati na kwamba chama hakitavumilia
viongozi wa namna hiyo huku akiwataka viongozi waliochaguliwa katika nafasi
mbalimbali kuhudhuria vikao na kushiriki shughuli zote zinazowahitaji bila
kuwepo visingizio vya utoro
Salome Kipondya ni mwenyekiti wa UWT wilaya ya Ilemela,
Amempongeza mbunge wa jimbo hilo Mhe Dkt Angeline Mabula pamoja na kumkabidhi
cheti kama ishara ya kutambua na kuthamini mchango wa mbunge huyo katika
shughuli za maendeleo na kuimarisha chama na jumuiya zake huku akiwataka
wanawake kuendelea kuungana mkono ili waweze kujikwamua kiuchumi na kushika
nafasi mbalimbali za uongozi katika Serikali
Nae katibu wa UWT wilaya ya Ilemela Bi Arafa Njechele amewataka
madiwani wa viti maalum kuhakikisha wanakutana na wanawake wote wanapofanya
ziara katika ngazi ya kata na matawi badala ya kuonana na wajumbe wachache ili
kuzuia mianya ya rushwa na mpasuko usio na sababu katika jumuiya
Jumuiya ya UWT wilaya ya Ilemela imefanya
kikao chake cha baraza la kawaida ambapo walikabidhi cheti kwa mbunge wa
jimbo la Ilemela Dkt Angeline Mabula kama ishara ya kutambua mchango wa mbunge
wa jimbo hilo na kisha kuzindua kamati za kampeni kuelekea uchaguzi wa Serikali
za mitaa mwaka 2024 pamoja na kamati ya kupinga ukatili na unyanyasaji
kwa ngazi ya wilaya
