Ndoto yangu 2024 ni kutetea taji la Olimpiki mjini Paris – Eliud Kipchoge
Lynne
Wachira
Kenya
Bingwa mara mbili wa
michezo ya Olimpiki katika mbio za marathon, Eliud Kipchoge
ametangaza rasmi kuwa atafungua msimu wa mwaka ujao mnamo mwezi Machi kwenye
mbio za mji mkuu wa Tokyo, nchini Japan.
Huku michezo ya Olimpiki ikifanyika mwaka ujao mjini Paris,
wengi wamekuwa wakisubiri kuona bingwa mtetezi wa Marathon angechagua mbio zipi
kabla ya kujitosa ulingoni kutetea taji lake.
“Ninajivunia sana kupata nafasi kushiriki mashindano ya
Tokyo, nilizichagua mbio hizi haswa kwa sababu zinafanyika mapema mwakani, ina
maana kuwa nitapata muda wa kutosha kupumzika na kuanza maandalizi ya olimpiki
huku mwaka ukiwa ungali mchanga.” Kipchoge aliiambia TRT Afrika Swahili kutoka
kambi yake ya mazoezi nchini Kenya.
Kipchoge atakuwa anarejea mjini Tokyo kwa mara ya pili
baada ya kushiriki na kutwaa ushindi katika Mbio za 2021 kwa kutumia muda wa
2:02:40.
Tokyo Marathon ni kati ya mashindano mengine ya miji
mikuu kama vile London, New York, Boston, Chicago, na Berlin, yakiwa ndiyo
mashindano ya ngazi ya juu zaidi katika mbio za Marathon.
“Mbio za Tokyo zina maandalizi ya hali ya juu sana lakini
zaidi ya hayo nina kumbukumbu nyingi nzuri kutoka Tokyo na Japan kwa jumla,
haswa ikizingatiwa kuwa mafanikio yangu yote ya mwaka wa 2021 niliyapata nchini
humo, nilishinda mashindano ya mji wa Tokyo mwezi Machi na baadaye nikawa
bingwa wa olimpiki mara mbili baada ya kushinda katika michezo ya Olimpiki ya
Tokyo.”
“Inapendeza sana kufahamu kuwa nitapata nafasi ya
kutangamana na mashabiki wa riadha kwani ilikuwa vingumu kwa waandalizi
kushirikisha mashabiki kwa sababu za kanuni zilizowekwa kukabiliana na janga la
Uviko -19 mwaka 2021.”
Iwapo Kipchoge atafanikiwa kutetea taji lake la Olimpiki,
basi ataandika historia kama mwanariadha wa kwanza kabisa wa Marathon kutwaa
ubingwa wa olimpiki mara tatu.
“Ndoto yangu ni kuibuka bingwa wa Olimpiki, itakuwa ni
raha isiyo kifani kutimiza ndoto hii mjini Paris, ninafanya juhudi kuhakikisha
kuwa maandalizi yangu yatakuwa ya kiwango cha juu.”
Kipchoge ni kati ya kikosi cha Olimpiki ambacho kilitajwa
hivi majuzi na shirkisho la riadha nchini Kenya – kikosi hicho cha wanariadha
kumi kitapunguzwa hadi wanariadha watatu ifikapo mwaka ujao.
Wengi watakuwa wanafuatilia kwa karibu mashindano ya
Kipchoge mjini Tokyo haswa baada ya rekodi yake ya dunia kuvunjwa na Mkenya
mwingine, Kelvin Kiptum katika mbio za mji mkuu wa Chicago mwezi Oktoba.
Mwaka huu Kipchoge
alishiriki mbio za Boston Marathon mwezi Aprili ambapo alimaliza katika nafasi
ya sita kabla ya kujinyanyua na kushiriki mbio za mji mkuu wa Berlin mwezi
Septemba ambapo aliandikisha historia kama mwanariadha wa kwanza kushinda mbio za Berlin mara tano.
