Polisi Tanzania yasema haina taarifa ya kuteswa kwa mtuhumiwa, yaahidi kuchunguza
Martin Otieno, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma.
................................................
NA, MWANDISHI WETU
BANDA MEDIA ONE.COM, DODOMA
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma Martin Otieno, amesema hana taarifa za kukamatwa na kuteswa na polisi kwa Kalamba Mnenge, mkazi wa kata ya Makole mkoani Dodoma kama ilivyoarifiwa na vyombo kadhaa vya habari hapo awali.
Hata hivyo, kamanda huyo wa polisi ameahidi kuzifanyia uchunguzi taarifa hizo akisema, iwapo itabainika, basi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya walio husika.
Kauli hii inakuja, siku kadhaa baada ya kusambaa kwa taarifa katika mitandao ya kijamii za kukamatwa kwa Kalamba Mnenge, mkazi wa Nyumba za Nation Houseng, Kata ya Makole Jijijini, Dodoma aliyedai kukamatwa na hatimae kufikishwa katika kituo cha Polisi cha Nkuhungu jijini humo ambapo inadaiwa aliteswa na kudhalilishwa.
Mnenge, mwenye umri wa miaka 38, na ambae ni mfugaji, ameelezea baadhi ya masaibu aliyopitia kuwa ni pamoja na kufungwa pingu miguuni na kutupiwa kwenye gari pamoja na kupigwa katika sehemu mbalimbali za mwili wake.
“Walifunga pingu miguuni na mikoni na kisha kunitupia kwenye gari lao na wakati wote sikujua ni wapi naeleka, lakini kuna sehemu walisimama na kupakia magunia ya mkaa na nilipochungulia niligundua wamenipeleka kituo cha polisi cha Nkuhungu,” anasema.
Hata hivyo, baadae, Mnenge, anasema alipitia masaibu mbalimbali ya mateso, na hatimae kuambiwa kuwa anakabiliwa na tuhuma za kuvunja duka na kuiba. Mnenge, ambae baada ya siku tatu aliachiliwa kwa dhamana, amezikanusha tuhuma hizo.
Halphan Mayagila, ambae yuko karibu na Mnenge anasema visa alivyopitia mwenzake vinawaacha na maswali mengi ya ueledi wa jeshi la polisi katika utendaji kazi wao.
Simulizi ya kalamba haitofautiani sana na ile ya Kurwa Raimond, ambae ni kijana mwenye umri wa miaka 36, yeye pia alifungwa kwa kutumia nyaya kabla ya kuburuzwa kiasi cha kuharibu kabisa ngozi yake ya mgongoni na baadaye askari kusema ana kichaa.
“Nilifungwa kwa nyaya na kuanza kupigwa. Polisi walisema mimi ni kichaa kwani waliniburuza chini kama mbwa na kisha nikalazimika kukubali mimi ni kichaa ili nisiendelee kupigwa,” alisema.
“Jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya kulinda mali za raia na haki zao haijalishi waliomkata ametenda kosa au la, hiyo haitoi nafasi kwa jeshi la polisi kuvunja haki za binaadamu” alisema Halpan.
“Matumani yangu ni kupata msaada wa kisheria kwa sababu nimetendewa sivyo bila kosa lolote na wakati wote huo wa kuwepo polisi, mifugo yangu kama bata, na kuku imepotea na nimemkuta ndama amekufa kwa sababu hakunyonya” alisema Mnenge huku akionekana kuvuta pumzi kwa shida.
Asha Othman ambae ni mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa eneo hilo amethibitisha kukamatwa kwa mkazi huyo na kusema imetengenezwa taswira isiyokubalika kwa Jeshi la Polisi.
Kwa upande wake, Dorice Mhagama ambae pia ni mkazi wa Dodoma, anadai kushuhudia tukio hilo, anasema, hatua zinazoweza kuchukuliwa na serikali ni kuhakikisha inadhibiti matukio kama hayo.
“Askari wametukosea na kutupa hofu kwamba polisi sio watu wa kawaida tena, wanaliharibia Jeshi la Polisi kwa sababu najua wanafahamu sheria lakini sijui imekuaje,” anasema Dorice.
Wakati wito ukitolewa kwa serikali kukomesha na kuwachukulia hatua baadhi ya wanaoonekana kukiuka misingi ya kazi, Kamanda wa jeshi la polisi mjini Dodoma amesisitiza kwamba hatua zitakuchuliwa.
“Sisi kama Jeshi la Polisi kuna hatua tunazochukua. Kwanza tukishapokea malalamiko ya mlalamikaji tutachunguza na tukibaini kuna mtendaji wetu amekwenda kinyume na maadili ya Jeshi la Polisi hatua za kisheria zitachukuliwa na wakati mwingine tukibaini tunakwenda mbali zaidi kwa kumfukuza kazi na kumfikisha Mahakamani,” amesema Otieno.

.jpeg)
