Barala la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana Jumatatu kujadili mzozo kati ya Ethiopia na Somalia. / Picha kutoka UN /Eskinder Debebe.
................................................................
Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
watakutana kwa mashauriano ya faragha ili kujadili hali ya mgogoro kati ya
Ethiopia na Somalia chini ya kipengele cha ajenda ya "Amani na Usalama
Afrika."
Ufaransa ambayo ndiyo rais wa baraza hilo, imepanga
mashauriano baada ya Somalia kuomba mkutano wa dharura katika barua ya Januari
23 kwa Baraza hilo.
Katika barua hiyo, Somalia imetaja Kifungu namba 35
cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambacho kinasema kuwa nchi yoyote mwanachama
wa Umoja wa Mataifa “inaweza kuwasilisha mzozo wowote, au hali yoyote...(yaani,
ambayo inaweza kusababisha msuguano wa kimataifa au kuzua mzozo) mbele ya
Baraza la Usalama au Baraza Kuu.”
Ombi la Somalia katika mkutano wa Baraza la Usalama
linakuja huku nchi hizo zikikataa mkataba ambao ulitiwa saini kati ya nchi
jirani yake ya Ethiopia na eneo la Somaliland.
Mkataba huo unakubali Ethiopia kukodisha sehemu ya
ukanda wa ufuo wa bahari katika Bahari Nyekundu kutoka Somaliland, lakini
Somalia imekataa ikidai kuwa Somaliland ni sehemu ya Somalia na Ethiopia haifai
kuingia mikataba nayo.
Somaliland ni eneo la kaskazini mwa Somalia ambalo
limejitambulisha kuwa huru lakini halitambuliwi na Umoja wa Afrika wala Umoja
wa Mataifa.
Katika barua yake ya Januari 23 kwa Baraza la Umoja
wa Mataifa, Somalia imesema kuwa makubaliano hayo, "yanafanya ukiukwaji
usio halali" wa mamlaka na uadilifu wa eneo la Somalia, ambalo Somaliland
"ni sehemu yake."
Ethiopia kwa upande wake imesema iko na haki ya
kupanga ufuo wa bahari kwani haina bahari wala bandari.
Mzozo huo ulichukua sura mpya wakati Ethiopia
ilipokataa kuhudhuria mkutano wa Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo IGAD ambayo
ilikuwa imepanga kuongelea suala hilo. Ethiopia na Somalia ni wanachama wa
IGAD.
Ethiopia ilitoa taarifa siku chache kabla ya mkutano
huo wa marais wa nchi wanachama uliofanyika 17 Januari nchini Uganda, ikidai
kuwa mkutano huo uliitishwa ndani ya muda mfupi na pia nchi hiyo ilikuwa na
majukumu mengine siku hiyo ya mkutano.

