Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi alipotembelea Banda la Wadau wa Haki Jinai kwenye Maonesho ya Wiki ya Sheria jijini Dodoma.
Na Lydia Churi-
Tume ya Utumishi wa Mahakama, Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na
Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewataka
wadau wa utoaji haki nchini kuwa waadilifu wanapotekeleza majukumu yao ya
kuwahudumia wananchi.
Akizungumza mara baada ya
kutembelea mabanda mbalimbali kwenye Maonesho ya wiki ya Sheria yanayoendelea
katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma, Dkt. Feleshi alisema Uadilifu,
Weledi na Uwajibikaji kama ilivyo salaam inayotumiwa na Mahakama ya Tanzania ni dhana ambayo haikwepeki katika zama hizi na hasa kwenye suala zima la utoaji
wa haki.
”Uadilifu ni jambo ambalo kila
Mtanzania anapaswa kulibeba na hasa kwa wale wanaofanya kazi za utoaji haki”,
alisisitiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamishna wa Tume.
Aidha, Dkt. Feleshi alisema amefurahishwa
na uwepo wa banda linalowakutanisha Wadau wa Haki Jinai kwenye Maonesho hayo na
kwamba uwepo wa banda hilo ni kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa
maadhimisho ya Wiki ya Sheria.
“Mimi ni Mjumbe ya Kamati ya
Maboresho ya Mfumo wa haki jinai nakiri kufurahishwa na uwepo wa banda la Wadau
wa Haki jinai ambapo nilipowatembelea wote wametoa maelezo ya namna taratibu
zinavyotakiwa kuwa, na ni kwa jinsi gani utekelezaji wa mapendekezo ya mfumo wa
haki jinai unafanyika,” alisema.
Alisema Maonesho ya Wiki ya
Sheria yamekuwa ya mafanikio kwa kuwa kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wadau wanaoshiriki
katika kutoa elimu. Kamishna huyo wa Tume amewataka wananchi kujitokeza kwa
wingi kwenye maonesho hayo ili kupata elimu ya sheria na kuwasilisha malalamiko
yao.
“Kwanza napenda kuishukuru
Mahakama ya Tanzania kwa kutualika sisi wadau wake kushiriki katika maonesho
haya, napenda pia kukiri kuwa mwitikio wa wadau katika maonesho haya ni mkubwa,
hivyo nitoe rai kwa wananchi wenye malalamiko kujitokeza,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mwanasheria
Mkuu wa Serikali ameipongeza Mahakama kwa kuzindua Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri
(TTS) ambapo alisema mfumo huo utasaidia kuwapunguzia Majaji na Mahakimu kazi
kubwa wanayofanya ya kuandika na kuwezesha uamuzi kwa haraka zaidi. Aliongeza
kuwa mfumo huo pia utaongeza uwazi na kupunguza malalamiko.
Maonesho ya Wiki ya Sheria
yanaendelea hadi tarehe 30 Januari, 2024 na kilele cha Siku ya Sheria kitafanyika
tarehe 01 Februari, 2024 ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.