Wanaharakati hao waliingia katika mitaa ya mji mkuu
wakiwa na mabango huku wengine wakiwa na majina na picha za waathiriwa.
"Acheni kutuua," waliimba huku
wakiandamana kuelekea bungeni, na hivyo kusimamisha msongamano wa magari katika
eneo kuu la biashara la Nairobi.
Takriban wanawake 16 wameuawa nchini Kenya mwaka
huu, kulingana na ripoti za vyombo vya habari, zikiangazia unyanyasaji dhidi ya
wanawake ambao serikali imeelezea kuwa "unaongezeka".
Genge la wanyang'anyi
Katika mojawapo ya visa vilivyopata umaarufu nchini
kote, mwanamke mwenye umri wa miaka 26 aliuawa mnamo Januari 4 katika nyumba ya
kukodisha ya muda mfupi na mshukiwa ambaye polisi wanasema ni sehemu ya genge
la unyang'anyi ambalo linalenga wanawake kupitia tovuti za uchumba.
Takriban wiki mbili baadaye, mwanamke mwenye umri
wa miaka 20 alinyongwa, kukatwa vipande vipande na mabaki yake kuingizwa kwenye
mfuko wa plastiki.
Wanaume wawili wanazuiliwa na polisi kuhusiana na
kesi hiyo lakini bado hawajafunguliwa mashtaka.
"Mauaji ya wanawake ni dhihirisho la kikatili
zaidi la unyanyasaji wa kijinsia," kitengo cha Amnesty International cha
Kenya kilisema katika taarifa kabla ya maandamano hayo.
Kuharakisha uchunguzi
"Haikubaliki na haipaswi kamwe kuwa ya
kawaida," shirika la haki za binadamu lilisema, likitoa wito kwa mamlaka
kuharakisha uchunguzi na kufunguliwa mashtaka kwa wahusika.
Katika maandamano ya Jumamosi, Terry Wangare, afisa
wa mawasiliano, alisema "wakati umefika kwa Kenya kusimama na kufanya
uamuzi".
"Hakuna anayejali. Ikiwa unalalamika, wewe ni
mbaya," kijana huyo mwenye umri wa miaka 32 aliiambia AFP.
Mwanafunzi wa umri wa miaka 23 Faith Claire Wanjiru
ambaye alikuwa kwenye maandamano yake ya kwanza alisema "alikuwa na
hasira" na hatakubali vurugu hizo.
"Kuchukua maisha ya mtu haipaswi kuwa kazi ya
mtu yeyote," alisema.
Ukatili wa kijinsia
Zaidi ya 30% ya wanawake nchini Kenya wanakumbana
na ukatili wa kimwili na 13% wanapitia aina fulani ya ukatili wa kingono,
kulingana na ripoti ya serikali iliyotolewa mwaka jana.
Kulikuwa na takriban visa 152 vya mauaji ya
wanawake nchini Kenya mwaka jana, kulingana na takwimu za shirika lisilo la
faida la Femicide ambayo huweka hesabu ya matukio yaliyoripotiwa pekee.
Mnamo 2022, wanawake na wasichana wapatao 725
waliuawa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki, kulingana na ripoti kutoka Ofisi
ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC).
