Sudan yamuita balozi wake wa Kenya baada ya ziara ya Dagalo
Kamanda wa kijeshi wa kikundi cha Rapid Support Forces, Mohamed Hamdan Dagalo, alikutana na rais Willima Ruto jijini Nairobi tarehe 3 Januari mwaka 2024. Picha. Ikulu Kenya
.................................................................................................
Sudan imemrudisha nyumbani balozi wake kutoka Nairobi
kama ishara ya kupinga kitendo cha Rais wa Kenya William Ruto kuandaa
mazungumzo na kamanda wa kijeshi wa kikundi cha Rapid Support Forces, Mohamed
Hamdan Dagalo, kaimu waziri wake wa mambo ya nje amesema.
Mkutano huo ulikuwa tarehe tatu mwezi Januari mwaka huu,
jijini Nairobi,
Dagalo, ambaye vikosi vyake vimekuwa vitani na jeshi la
serikali ya Sudan linaloongozwa na Abdel Fattah al-Burhan tangu Aprili, amekuwa
akizuru miji mikuu ya Afrika katika ziara yake ya kwanza nje ya nchi.
Tayari alitembelea Uganda, Ethiopia na Djibouti pamoja na
Kenya, na kwa sasa yuko Afrika Kusini,jambo amabalo halimfurahishi jenerali Al
Burhan.
Katika taarifa iliyotolewa na shirika rasmi la habari la
SUNA la Sudan, siku ya Alhamisi, kaimu waziri wa mambo ya nje wa Sudan Ali
al-Sadiq alisema balozi huyo ameitwa "kwa mashauriano ya kupinga mapokezi
rasmi yaliyoandaliwa na serikali ya Kenya..."
Vita vya mauti
Alisema mashauriano hayo "yatashughulikia uwezekano
wote wa matokeo ya uhusiano wa Sudan na Kenya."
Uhusiano kati ya Burhan na serikali ya Kenya umedorora
kwa miezi kadhaa, huku Nairobi ikijaribu kuweka njia za mawasiliano wazi na
Dagalo ili iweze kupatanisha katika mzozo huo.
Vita vya Sudan vimewauwa zaidi ya watu 12,190, kulingana
na makadirio ya kihafidhina kutoka kwa Mradi wa 'Armed Conflict Location and
Event Data' Project. Zaidi ya watu milioni saba wamelazimika kukimbia makazi
yao, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.
Juhudi za upatanishi zimesimama kwa kiasi kikubwa.
