TBS YAINGIA MAKUBALIANO NA JESHI LA POLISI KUKAGUA MAGARI YANAYOTUMIKA NCHINI
Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt.
Athuman Ngenya akiwa pamoja na Mkurugenzi wa
Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna wa Polisi Awadhi Haji
wakisaini makubaliano (MoU) katika kushirikiana katika
ukaguzi wa Vyombo Vya Moto kwa kutumia Vifaa vya Kisasa vinavyomilikiwa na TBS.
Hafla hiyo imefanyika leo Januari 5,2024 Jijini Dar es Salaam.
*************
NA
EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
SHIRIKA
la Viwango Tanzania (TBS) limesaini Hati ya Makubaliano (MoU) na Jeshi la
Polisi ili kushirikiana katika ukaguzi wa Vyombo Vya Moto kwa kutumia Vifaa vya
Kisasa vinavyomilikiwa na TBS.
Akizungumza
na Waandishi wa habari leo Januari 5,2024 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa
TBS, Dkt. Athuman Ngenya amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kutekeleza
azma ya kuendelea kulinda Maisha ya watanzania kwa kuhakikisha kuwa ukaguzi wa
magari wakati yanapotumika hapa nchini unaofanyika kwa mujibu wa Sheria ya
Trafiki (yaani Road Traffic Act, Cap 168), unafanyika kwa kutumia mitambo ya
kisasa ili kuthibitisha usalama wake.
"Kwa
kuzingatia uwezo uliopo,TBS itatumia wataalam wake, viwango pamoja na mitambo
ya kisasa katika kukagua na kupima magari yote yatakayoletwa na Jeshi la
Polisi, Kitengo cha Trafiki kwa ukaguzi kwa mujibu wa Sheria Usalama
Barabarani Sura 168 ambayo inalazimu kufanyika ukaguzi wa vyombo vya moto ili
kuhakikisha vinakidhi matakwa ya vigezo vya usalama kwa lengo la kulinda
usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara". Amesema
Aidha
amelihakikishia jeshi la polisi kwamba TBS ni mshirika sahihi wa Jeshi la
Polisi Tanzania, kwani ndiyo inayodhibiti ubora na usalama wa vyombo vya moto
vinavyoingia nchini.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini,
Kamishna wa Polisi Awadhi Haji amesema kupitia makubaliano hayo wanatarajia
usalama barabarani kuimarika zaidi kwa watumiaji wa barabara.
"Tukiwa
na Vyombo vya Moto salama tutakuwa na watumiaji salama wa barabara, tutakuwa na
barabara salama na pia shughuli za uokozi zinaweza kuimarishwa na mwisho
tutakuwa na tumeimarisha uongozi katika usalama barabarani". Amesema
Amesema
kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa Maelekezo ya Tume ya Haki Jinai inayosisitiza
kushirikiana na wadau mbalimbali katika usimamizi wa sheria za usalama
barabarani ili kuzuia uhalifu barabarani.
Pamoja
na hayo amewataka wamiliki wa vyombo vya moto kuhakikisha wanatimiza wajibu wa
kisheria wa kukagua vyombo vyao kama inavyoelekezwa katika sheria kwani jeshi
la polisi litakuwa na muhari kwa watakaoshindwa kutii sheria bila shuruti.




