Na Mwandishi wetu, Mwanza
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony
Mavunde amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini imedhamiria kuweka
mikakati ya kuongeza ushiriki wa watanzania katika shughuli za
madini ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya watanzania wanaotoa huduma na
usambazaji wa bidhaa migodini sambamba na kufungamanisha Sekta ya Madini na
sekta nyingine muhimu za kiuchumi.
Aidha, amesema kuwa Wizara ya Madini
kupitia Vision 2030 ya Madini ni Maisha na Utajiri inatarajia kufanya utafiti
wa kina wa madini nchi nzima utakaoondoa uchimbaji wa madini wa kubahatisha na
kuongeza uwekezaji katika Sekta ya Madini ikiwemo idadi ya kampuni kubwa
za uchimbaji wa madini zitakazopelekea ongezeko la watoa huduma kwenye migodi
ya madini, ushiriki wa watanzania na Sekta Binafsi.
Waziri Mavunde ameyasema hayo leo
Januari 05, 2024 jijini Mwanza kwenye ufunguzi wa kikao chake na watoa huduma
kwa wamiliki wa leseni za madini walioshiriki katika kikao hicho kilichohusisha
pia Taasisi za Fedha, Vyama vya Wachimbaji wa Madini, Taasisi za Umma, Wizara
ya Madini na Taasisi zake.
“Dhamira ya Serikali kupitia
Wizara Madini ni kuongeza ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini, mapato
ya nchi kuongezeka na kuwa Sekta inayoongoza katika mchango katika uchumi wa
nchi,” amesisitiza Waziri Mavunde.
Ameongeza kuwa nia ya Serikali ni
kuona watoa huduma wanazalisha bidhaa bora nchini na kuwataka kuungana na
kuwa na nguvu ya pamoja kwenye uzalishaji ili kutosheleza mahitaji makubwa ya
kampuni za madini nchini.
“Nipo hapa tuzungumze, kupromote
uzalishaji wa bidhaa za ndani, lazima tubadilishe jambo hili, ni eneo ambalo
nitalisimamia kwa dhati, vitu vingi bado vinaagizwa nje, tunaweza kuwajengea
uwezo watu wetu ili wazalishe ndani na huu ndio utaratibu wetu sisi. Ninataka
kuacha alama katika eneo hili, nipo tayari kupokea changamoto za kisheria
na kikanuni na kuzifanyia kazi,” amesisitiza Waziri Mavunde.
Kufuatia hali hiyo, ametoa rai kwa
Taasisi za Fedha kuwawezesha watanzania kimitaji ili waweze kushiriki katika
Uchumi wa Madini na kuongeza kwamba, Serikali ipo tayari kuwaonesha fursa
zilizopo katika Sekta ya Madini na namna wanavyoweza kushiriki.
Pia amewataka wadau wa madini nchini
kujipanga kwenye uwekezaji katika madini ya kimkakati kwa kuwa mahitaji yake
yanaendelea kuongezeka duniani.
“Mfano mahitaji ya madini aina ya
kinywe (graphite) yanatarajiwa kufikia asilimia 500 kwenye uchumi wa dunia
ifikapo mwaka 2050 na madini haya tunayo, hivyo ni vyema tukaanza kujipanga
kwenda kwenye uchumi shindani.” amesema Waziri Mavunde.
Awali, akielezea mafanikio ya
utekelezaji wa Kanuni za Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini za
mwaka 2018, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba
ameeleza kuwa ni pamoja na ongezeko la ajira kwenye migodi kutoka 6,668 kati ya
7,003 ikiwa ni asilimia 95 mwaka 2018 hadi kufikia 16,462 kati ya 17,024 sawa
na asilimia 97 kwa mwaka 2022 na ongezeko la manunuzi ya huduma na bidhaa kwa
kampuni za kitanzania kutoka Dola za Marekani milioni 756.63 ambayo ni sawa na
asilimia 62 ya manunuzi yaliyogharimu kiasi cha Dola za Marekani Milioni
1,228.38 kwa mwaka 2018 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 1.08 ambayo ni
sawa na asilimia 86 ya kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.25 ya manunuzi yote
yaliyofanyika mwaka 2022.
Ameongeza kuwa, kumekuwepo na
ongezeko la ushiriki wa watanzania kwenye nafasi za menejimenti kwenye migodi
ya madini tofauti na kabla ya kuanzishwa kwa utekelezaji wa kanuni za ushiriki
wa watanzania katika sekta ya madini.







