Jinamizi barabarani: Mwamko mpya wa kupunguza vifo Afrika
Gift
Dumedah Ghana
Mwaka mpya umefika na bila shaka, malengo ya wana Afrika
yanabaki kuwa yaleyale; kutafuta suluhu ya majanga yatokanayo na ajali za
barabarani.
Kwa hakika, bara la Afrika limejiwekea malengo mahususi,
ya kumaliza ajali barabarani zinazosababisha watumiaji kupata majeraha na
hatimaye kupoteza maisha.
Kimsingi, bara la Afrika limeweka malengo la kuhakikisha
usawa na usalama katika huduma za usafiri kwa watu wake.
Iwapo Afrika imenuwia kuukuza mkakati huu,
itajihakikishia kuokoa maisha ya watu 27 kwa kila watu 100,000; na takriban
asilimia 7 ya Pato la Taifa la kila mwaka (GDP) kwa nchi nyingi barani.
Hata hivyo, makisio haya hayajumuishi madhara ya
kisaikolojia kwa waathirika wa ajali za barabarani.
Takribani watu 3,609 walipoteza maisha kwa ajali za
barabarani nchini Kenya. Vifo hivyo viliripotiwa kati ya mwezi Januari na
Oktoba mwaka jana.
Vivyo hivyo, watu 1,839 waliangamia barabarani na wengine
12,678 kujeruhiwa nchini Ghana.
Kwa mujibu wa
Shirika la Afya Duniani (WHO), nchi za Nigeria, Ethiopia, Afrika Kusini na
Sudan zikiongoza kwa jinamizi la ajali za barabarani, kusini mwa jangwa la
Sahara.
Kadhalika, nchi
ya Nigeria ndio kinara wa vifo vitokanavyo na ajali za barabarani.
Nchi hiyo,
ambayo ni ya tatu kwa uzalishaji wa mafuta barani Afrika, ina kiwango cha juu
cha vifo 52.4 kati ya 100,000 kwa kila nchi duniani. Msumbiji inafuata kwa
karibu vifo 46.7 kati ya watu 100,000 duniani.
Jukumu la pamoja
Ni ukweli
usiopingika kuwa jukumu la kupunguza jinamizi kwenye barabara nyingi
linawezekana kwa sababu ajali za barabarani zinaepukika. Ukweli huu unakuja
wakati WHO inaripoti kuwa vifo vitokanavyo na ajali za barabarani, kati ya 2010
na 2021 vinapungua, isipokuwa kwa bara la Afrika ambalo limeshuhudia asilimia
17 tu ya upungufu huo, ilhali idadi ya vyombo vya moto na miundombinu ya
barabara bado chache na duni, ikilinganisha na mabara mengine.
Ni ukweli
usiopingika kuwa, kutokana na hali ya uchumi barani Afrika, wananchi wengi
huagiza vyombo vya moto kutoka ng’ambo na asilimia kubwa ya magari hayo
hayakidhi vigezo vya matumizi ya barabarani.
Ripoti ya
Shirika la Afya Duniani inaeleza bayana kuwa hatua kubwa inapigwa katika nchi
zilizoamua kupitisha mifumo salama ya matumizi ya barabara.
Mifumo hiyo
imeweka msisitizo kuwa usalama ni wajibu wa kila mmoja wetu; kutoka kwa
watumiaji wa barabara, wasimamizi wa barabara, wabunifu, wajenzi, watunzaji wa
mfumo wa barabara na watoa huduma baada ya ajali.
Mfumo huo
unaongozwa na misingi mikuu mitano ambayo inasisitiza kuwa: vifo na majeruhi wa
barabarani havikubaliki, watu hufanya makosa barabarani, watumiaji wa
barabaraba huwa kwenye mazingira hatarishi ya ajali, kuwa ni vyema kuchukua
hatua ili kupunguza ajali vyengine na umuhimu wa kutoa suluhisho kwa viashiria
vipya vya ajali.
Kwa kuzingatia
kanuni na vipengele hivi, mbinu ya mfumo salama inalenga kuunda mazingira
salama ya barabarani na kupunguza idadi ya ajali za barabarani, vifo na
majeruhi.
Namna ya kusamehe makosa
Kando na
mtazamo wake unaolenga matokeo, mfumo salama ni mbinu pana yenye vipengele vya
kipekee.
Inalenga
binadamu, ikizingatia usalama wa watumiaji wa barabara kwa kufanya mabadiliko
kwa matumizi ya vyombo vya moto na muundo wa barabara huku ikishughulikia na
kuzingatia kasoro za kibinaadamu.
Mbinu hii pia,
inabeba mtazamo wa mfumo mzima kwa kushughulikia mifumo, sera, na mazingira
halisi, ikiwa ni pamoja na muundo wa barabara, muundo wa gari na usimamizi wa
kasi.
Mbinu hiyo
hutumia muundo wa kusamehe makosa kwa kusisitiza kuwa mfumo wa usafirishaji
unapaswa kuundwa na kuendeshwa ili kupunguza madhara, huku ikikubali kuwa
watumiaji wa barabara hufanya makosa na wakati mwingine maamuzi mabaya.
Na pia kwamba,
mwili wa binadamu una kikomo cha kuvumilia ajali za barabarani kabla ya vifo au
majeraha makubwa.
Hatari zaidi kuliko magonjwa
Mbinu ya mfumo
salama hutumika kushughulikia masuala ya usalama yanayohusiana na miundombinu,
tabia ya binadamu, uangalizi unaowajibika wa sekta ya magari na uchukuzi, na
majibu ya dharura.
Pamoja na
matokeo chanya ya mfumo huo, bado nchi nyingi za Kiafrika zinashindwa
kuutekeleza.
Kimsingi, kuna
masuala mtambuka na changamoto kadhaa zinazofanya nchi nyingi Afrika kushindwa
kuupitisha mfumo huu, kama sio kuufanya sehemu ya maisha yao ya kila siku.
Sababu kuu kati
ya nyingi ni kuwa suala la usalama barabarani halijapewa kipaumbele katika nchi
nyingi za Kiafrika, na bado halionekani kama ni tatizo.
Hii
inadhihirishwa na rasilimali finyu zinazotengwa katika kukuza usalama
barabarani na kupunguza majeraha.
Kwa mfano,
mpango mkakati wa usalama barabarani Afrika unazitaka nchi za Afrika kutenga
angalau asilimia 10 ya uwekezaji kwenye miundombinu ya barabara kwenye usalama
barabarani.
Ingawa ni
vigumu kuthibitisha mgawanyo halisi wa kitaifa, bado kuna changamoto
zinazohusiana na rasilimali chache, vipaumbele vinavyoshindana, na dhamira ya
kisiasa.
Kulingana na
WHO, majeraha yatokanayo na ajali za barabarani ndiyo sababu kuu ya vifo baada
ya Malaria na Kifua Kikuu.
Hata hivyo,
bado haipewei msukumo unaostahili katika uwekezaji haswa wa rasilimali fedha,
miundombinu ifaayo na tafiti.
Kinachokosekana
Hata hivyo,
kuna fursa si haba kwa mwaka 2024 za kufanya maendeleo ya kweli kuhusu kukuza
usalama na kuzuia majeraha kupitia mbinu ya mfumo salama barani Afrika.
Idadi kubwa ya
miundombinu ya usafiri na uhamaji bado inajengwa barani Afrika, kwa matarajio
ya kuunganisha viwango vya usalama moja kwa moja.
Hata hivyo,
hili halitotegemea maajabu bila jitihada madhubuti na za kimakusudi.
Usalama wa
maisha ya binadamu lazima upewe kipaumbele kwenye barabara zetu.
Ahadi ya kuwa
na maono sifuri katika kuokoa maisha kwenye barabara zetu inaweza kufikiwa
kupitia mbinu ya mfumo salama. Hata hivyo, kipengele kinachokosekana ni hatua
za dhati kwa pande zote, yaani watumiaji wa barabara, watunga sera, wabunifu,
wajenzi, watunzaji wa mfumo wa barabara na watoa huduma za baada ya ajali.
Ni matumainio
ya kila muafrika wa kuwa na mfumo salama wa usafiri usio na vifo na majeraha
yanayohudumia watumiaji wote wa barabara.
Mwandishi wa Makala hii ni msomi kutoka Ghana ambaye
andiko tafiti yake imeangazia uhakika wa huduma za usafiri Afrika.

.jpeg)