WADAU WA TIBA ASILI NA TIBA MBADALA WATAKIWA KUSAJILI DAWA ILI ZITUMIKE KATIKA MFUMO RASMI WA HOSPITALI
.................................................................. Na
WAF - Dodoma.
Serikali imewataka waganga na wadau
wa tiba Asili nchini kusajili dawa wanazotengeneza ili ziingizwe katika mfumo
wa hospitali na kuongeza masoko ya huduma jumuishi za Afya kwa kufuata mfumo
rasmi wa muongozo wa dawa.
Wito huo umetolewa leo Januari 4,
2024 na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba asili Dkt. Marko Hingi wakati
alipomuwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu katika
kikao cha waganga pamoja na wakuu vyama vya tiba asili na tiba mbadala Jijini
Dodoma.
Katika kuendelea kuimarisha kada ya
tiba asili amesema Serikali imeingiza baadhi ya dawa za tiba asili katika
huduma jumuishi za Afya kwa kufuata mfumo rasmi wa muongozo wa dawa.
“Mpaka sasa Hospitali saba nchini
zimeanza kutumia dawa za tiba asili na mbadala kama Huduma jumuishi za Afya kusaidia
wananchi katika kupona magonjwa mbali mbali”. Amesema Dkt. Hingi.
Dkt. Hingi amesema kuwa ujenzi
wa kiwanda cha NIMR Mabibo umefikia asilimia 98 na unatarajia kukamilika mapema
mwaka huu.
“Kiwanda hicho kitakuwa ni jukwaa la
uzalishaji wa dawa za tiba asili na mbadala hapa nchini na kusambazwa katika
nchi za ukanda wa SADC“. Ameeleza.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Baraza
la Waganga wa Tiba Asili na Mbadala Prof. Hamisi Malebo amesema wana jukumu la
kuondosha na kutibu magonjwa mbalimbali katika jamii, kuleta amani na kuisaidia
Serikali kuifikia jamii.
