Walimu wanne wa shule za msingi zilizopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza pamoja na mfanyabiashara mmoja mkazi wa Wilaya ya Nyamagana wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kughushi nyaraka za watumishi wa serikali ili kupata mikopo katika taasisi mbalimbali za kifedha.
Akizungumza
mkoani Mwanza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa ameeleza
kuwa tukio hilo liliripotiwa kituo cha Polisi Misungwi Januari 4,2024 baada ya
kugundua kwamba baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi
wamesitishiwa makato ya mikopo yao wakati bado hawajamaliza kulipa madeni yao.
Baada
ya ufuatiliaji Jeshi la Polisi liliweza kubaini kuwa nyaraka za kusitisha
mikopo hiyo zilighushiwa na watumishi hao na kwenda kuomba mikopo mipya kwenye
taasisi nyingine huku wakijua bado wanadaiwa marejesho kwenye taasisi
walizokopa awali.
Watuhumiwa
waliopanga na kuratibu njama za kughushi nyaraka kwa lengo la kujipatia fedha
kwa njia isiyo halali ni Majaliwa Philipo Mwaikambo,(34),mfanyabiashara na
mkazi wa Nera Kata ya Isamilo ambaye ni mtuhumiwa sugu wa kughushi nyaraka.
Wengine
ni Magreth Michael Simba (42), Mwalimu wa shule ya msingi Ntende Wilaya ya
Misungwi,Mariam Ngwile (48),Mwalimu wa shule ya msingi Usagara Wilaya ya
Misungwi, Beatus Nyombi,(53),Mwalimu wa shule ya msingi Mbalama Wilaya ya
Misungwi na Jitashika Ezekiel Nchemba,(42),Mwalimu wa shule ya msingi Ntende
Wilaya ya Misungwi.
Katika
tukio jingine Mutafungwa ameeleza kuwa wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa sugu
wa usafirishaji na uuzaji wa dawa za kulevya ambao wamekuwa wakisafirisha
kupitia barabara ya Mwanza – Musoma kwa kutumia magari binafsi.
Ambapo
watuhumiwa hao ni Peter Charles kwa jina maarufu Peter Mirungi(50) mkazi wa
Igoma, Said Abdallah (27),mkazi wa Igoma na Emenn Gamariel kwa jina maarufu
Munuo (30),mkazi wa Igoma Wilaya ya Nyamagana.
Mutafungwa
ameeleza kuwa tukio hilo limetokea Januari 12,2024 majira ya saa 03:00 usiku
katika Kijiji cha Ilungu, Kata ya Kahangala Wilaya ya Magu ambapo Askari Polisi
wakiwa doria walifanikiwa kukamata magari mawili yakitokea Mkoa wa Simiyu na
baada ya kusimamisha gari namba T.481 AJZ Toyota Surf lililokuwa likiendeshwa
na Emenn Gamariel na lilipopekuliwa kulikutwa na vifurushi 17 vya dawa za
kulevya aina ya Mirungi.
Wakati
upekuzi ukiendelea ghafla lilitokea gari namba T. 406 EAM Toyota Alphard
likiendeshwa na Said Abdallah akiwa na Peter Charles mmiliki wa mirungi hiyo.
“Baada
ya mahojiano ilibainika kuwa gari namba T.406 EAM Toyota Alphard lilikuwa
likisindikiza gari namba T. 481 AJZ Toyota Surf lililokuwa limebeba shehena ya
Mirungi ili isikamatwe na Askari Polisi,”ameeleza Mutafungwa.
Watuhumiwa
wote wamehojiwa kwa kina na watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi
kukamilika.Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawataka wananchi kuendelea kutoa
taarifa za uhalifu na wahalifu ili ziweze kufanyiwa kazi kwa haraka pia
litaendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahalifu.
