Wanawake wazee wajifunza karate kupambana na uhalifu nchini Kenya
Job
Samuel
Nairobi, Kenya
Kutana na kikundi cha wanawake wazee 20 wa kenya
waliojifunza Karate kukabiliana na vitendo vya uwizi na ubakaji katika kijiji
cha Korogocho, jijini Nairobi nchini kenya.
Korogocho ni mojawapo ya vitongoji duni vilivyo na idadi
kubwa ya watu jijini Nairobi, ambapo ubakaji na wizi ulikuwa wa kawaida.
"Tulianzisha kikundi hiki mwaka 2007 tulipogundua
kuwa wanawake wazee walilengwa sana na wabakaji na waizi," Beatrice
Nyariara, Mwenyekiti wa kikundi cha Shosho Jikinge anasema.
Vitendo vya ubakaji vilikithiri katika eneo hilo, baada
ya baadhi ya vijana katika eneo hilo kuamini kwamba, kufanya mapenzi na
wanawake wazee kunaweza kutibu virusi vya Ukimwi, huku wengine wakiamini kuwa
kunaweza kuwaondolea mikosi.
Mdogo zaidi wa wanawake hawa wazee ana miaka 60 na yule
mwenye umri mkubwa akiwa na umri wa miaka 94. Ujuzi wao wa ngumi na kurusha
mateke wanasema umewafaa.
Msafiri mmoja kwa Jina ‘Jake’ aliyekuwa akitembelea eneo
hilo alipata fursa ya kuelezwa masaibu yaliyowakumba wanawawake na wanaume
wazee katika eneo hilo. Aliwahurumia na kuanza kuwapa mafunzo ya kuwalinda na
kuwaelimisha jinsi ya kupambana na mwizi au mbakaji.
’’Alituambia tuunde kikundi. Baada ya siku kadhaa,
alituletea mke wake. Mke wake alikua anakuwa na maarifa ya kupigana karate.
Alitufunza kwa muda wa miezi sita. Wiki mbili za kwanza tulikua na maumivu
makali, kwa sababu ya kufanya mazoezi. Miili yetu imezeeka. Karibu hata tuache
kufanya mazoezi," amesema Beatrice Nyariara, mmoja wa waanzilishi.
Walibuni jina la kikundi hicho na kujiita, ‘Shosho’ Jikinge.
’Shosho’ni jina la kabila moja nchini Kenya, lenye maana, 'bibi' au 'mwanamke
mzee.' Na hiyo ndio iliyokuwa maana halisi ya kikundi hivyo, ya kutaka wanawake
hao kujilinda.
Wana gunia la ndondi wanalotitumia kufanyia mazoezi.
Wamejifunza mahala pa kumpiga mhalifu na kisha kupiga mayowe wakiitisha
usaidizi.
Wamejifunza kuwa huwa wanampiga mhalifu teke sehemu ya
chini ya kiuno, katikati ya miguu, au kwenye pua ama utosini huku wakipiga
mayowe ya kuomba msaada.
Mafunzo hayo
pia yanawaelekeza kina mama hao, iwapo wangetaka kufanikiwa kujinusuru, jinsi
ya kuwashambulia washambuliaji kwa nguvu katika sehemu za mwili ambazo watawapa
maumivu mno.
Maneno yao,
wanayoyatumia pindi wanapovamiwa na vibaka ni kama, "Hapana! Wachana na
mimi! Niachilie! Njooni mnisaide jamani!" Wanasema hivyo huku wakijaribu
kukimbia kutoka eneo la uhalifu.
"Tunakuja
kufanya mafunzo kwa masaa mawili kwa siku, mara nne au tano kwa wiki. Baada ya
hapo kila mmoja wetu anaelekelea kutafuta chakula cha kila siku kusaidia
familia yake. Iwapo kuna yeyote pale nje ambaye pia angependa kutusaidia kwa
vyovyote vile, tutashukuru" anasema Grace Ngánga, mwanachama wa Shosho
Jikinge.
Kikundi cha wazee hao kina wanachama kuanzia miaka 60 hadi 94. Picha/TRT Afrika.
Maarifa kuhusu
mafunzo yanayoendelea kwa wanawake hawa yameenea kijijini kama moto msituni
wakati wa kiangazi. Hii imewafanya washambuliaji wengi kuogopa na baada ya muda
matukio ya ubakaji yanayowalenga wazee yamekua yakipungua.
’’Kikundi hiki
kimetusaida sana. Mazoezi yametupa nguvu. Wizi na ubakaji wa wazee umepungua.
Tumepata pia nguvu za kulima mashamba na kupanda mboga licha ya umri wetu.
Tutafunza hata wajukuu wetu kujilinda," anasema Rose Adhiambo, ambae pia
ni mwanchama wa Shosho Jikinge.
"Wiki mbili za kwanza tulikua na
maumivu makali, kwa sababu ya kufanya mazoezi. Miili yetu imezeeka. Karibu hata
tuache kufanya mazoezi."
Beatrice Nyariara, mwanachama wa Jilinde
Shoshoo
Wanawake hawa
sio kwamba wanajifunza tu kujilinda, lakini pia wana mpango wa kuweka akiba
ambao umewawezesha kuwa na biashara ndogo ya kutengeneza mikoba iliyotengenezwa
kwa mikono na mapambo ya shanga ambayo wanauza.
"Kila
wiki, tunatoa shilingi ishirini za Kenya. Fedha hizi kwa muda sasa
zimetuwezesha kutengeza mikoba hii. Angalau tunapata kitu hata kama ni kidogo.
Pia, mmoja wetu anapougua au kupata msiba, tunatoa mchango katika akiba yetu na
kumsaidia,“ anasema Nyariara huku akionekana mwingi wa mawazo.
Kina mama hawa wanasema, tangu kuanza kujifunza karate, uhalifu umepungua kijijini hapo. Picha/TRT Afrika.
Kulingana na
makadirio ya polisi nchini Kenya, asilimia 73 ya uhalifu wa kingono
hauripotiwi.
Kina mama hao
wanasema kwamba kunapokua na tukio au jaribio la wizi au ubakaji polisi na
usalama hukawia kufika sehemu ya tukio. Hii ndio sababu yao kuu iliyowafanya
kuchukua hatua ya kupata mafunzo ya kujilinda wao wenyewe.


