*Aliyosema Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan*
#Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeweka bayana kulindwa kwa taarifa binafsi za watu au kulindwa kwa haki za binadamu ikiwemo kulindwa kwa haki ya faragha.
#Tunapozindua Tume hii, sio tu tumetekeleza matakwa ya Katiba yetu bali pia tunatekeleza ahadi ya Ilani ya Chama Tawala ya 2020/2025 na kukamilisha wajibu wetu wa Kikanda na Kimataifa.
#Kwa kuzingatia maendeleo makubwa ya kiteknolojia, taarifa binafsi za watu zinaweza kukusanywa, kuchakatwa na kutumika bila hata wahusika kufahamu hivyo, hatuna budi kulindana. Kutokana na uhalisia huo, serikali imelazimika kuweka utaratibu wa kisera na kisheria ili kulinda taarifa binafsi za Watanzania.
#Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na taasisi imara ya usimamizi na ukusanyaji wa uchakataji wa taarifa hizo, ni nyenzo muhimu katika kujenga uchumi na mifumo ya kidijitali, Tume hii itambue kwamba ina kazi nzito na muhimu kwa maisha yetu ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
#Natoa maelekezo kwa Tume hii kuhakikisha taasisi zote za umma na binafsi zinapaswa kusajiliwa na kutekeleza Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi kabla mwezi Desemba, 2024.
#Natoa maelekezo kwa taasisi zinazokusanya na kuchakata taarifa binafsi zihakikishe zinazingatia matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, na Tume kutoa elimu kusisitiza wajibu wa taasisi hizo.
#Maafisa wa Tume mna kazi kubwa ya kufanya, nataka muifanye kwa weledi na ubora zaidi, ninyi ni wadhibiti lakini zaidi ninyi ni wawezeshaji. Nendeni mkafanye uwezeshaji ili watoa huduma mbalimbali waridhike na utunzaji wa haki binafsi nchini.
#Nataka Waziri mwenye dhamana na Tume hiyo kuhakikisha anafuatilia kwa ukaribu kazi za Tume, fuatilia ili malalamiko yatakayoibuliwa yashughulikiwe kwa haraka. Wizara ilete taarifa ya utekelezaji mara mbili kwa mwaka.
#Naitaka Ofisi ya Waziri Mkuu isimamie na kuhakikisha mifumo yote ya TEHAMA nchini inasomana, natoa agizo kuwa ifikapo Desemba, 2024 mifumo yote ya serikali iwe imesomana.
*Aliyosema Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye*
#Msimamo wako thabiti na usimamizi wako Rais Samia katika kuhakikisha sheria hii inatungwa na Tume hii inaundwa, ni ushahidi tosha wa namna unavyoheshimu utawala wa sheria na uumini wako mkubwa wa Katiba zetu.
#Natumia nafasi hii kumshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa namna ambavyo amekuwa sehemu ya mchakato wa kutungwa kwa sheria na kuanzishwa kwa Tume hii, mara kadhaa tumefanya nae vikao pamoja na wataalam wake kuhakikisha tunakuwa na mazingira bora ya utunzaji wa taarifa binafsi kwa taifa letu.
#Uwepo wa taasisi imara, ikiwemo Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ni moja ya vigezo vinavyoifanya Tanzania kuwa ya pili kwa usalama mtandaoni kwa bara la Afrika. Tukio hili la uzinduzi wa Tume hii, linaiingiza Tanzania katika orodha ya nchi za wastaarabu duniani ambao wanaheshimu utawala wa sheria, haki, ubinadamu, utu wa mtu na faragha za watu.
#Tume hii ni chombo muhimu katika kuhakikisha maslahi ya uwekezaji wa ndani na nje ya nchi yanazingatiwa na kufanyika kwa tija na malengo kusudiwa, pamoja na kuimarisha masuala ya usalama wa nchi.
#Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi inatarajiwa kuimarisha misingi ya demokrasia, utawala bora na utawala wa sheria. Mazingira haya yatazidi kuvutia uwekezaji wa ndani na nje kwani wawekezaji watakuwa na uhakika wa usalama wa taarifa zao.
#Utekelezaji wa Sheria ya ulinzi wa taarifa binfsi nchini, utasaidia wawekezaji wa ndani kupata fursa sawa katika kuwekeza katika nchi zingine, kwani watakuwa wanaaminika kutokana na nchi yetu kutekeleza makubaliano ya jamii ya kimataifa ya kuwa na sheria hii.
#Matumizi ya mfumo wa kusajili wakusanyaji na wachakataji wa taarifa binafsi pamoja na kushughulikia malalamiko dhidi ya ukiukwaji wa misingi ya ulinzi wa taarifa binafsi, utasaidia shughuli za Tume kutekelezwa kisayansi na hivyo kupunguza au kuondoa malalamiko kutoka kwa wadau wa ukusanyaji, uchakataji, uhifadhi na usambazaji wa taarifa binafsi.
#Mfumo huu wa kusajili wakusanyaji na wachakataji wa taarifa binafsi pia utajenga weledi kwa kupunguza mawasiliano ya moja kwa moja baina ya watumishi wa Tume na wadau.
*Aliyosema Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla*
#Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ina jukumu la kusimamia Sera ya Taifa ya TEHAMA ya Mwaka 2016, Sera hiyo imebainisha uwepo wa mifumo ya kisheria na kitaasisi ambayo itaweka mazingira wezeshi katika kuhakikisha TEHAMA inaendelea kuwa nyenzo muhimu katika kukuza uchumi wa kidijitali.
#Serikali imeridhia utungwaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Namba 11 ya Mwaka 2022, ambayo ilianza kutekelezwa Mei 01, 2023.
#Uwepo wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, una taswira ya kitaifa na kimataifa. Lengo la hafla hii ni kuujulisha umma kuwa Tume hiyo itaanza kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zinazohusu ulinzi wa taarifa binafsi.
#Tume hii imeweza kukamilisha uundwaji wa mfumo wa usajili na upokeaji wa malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa misingi ya ulinzi wa taarifa binafsi.
*Aliyosema Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Balozi Adadi Rajabu*
#Tayari tumeanza kufanya mikakati maalum ya kuweza kujenga na kutoa elimu kwa umma kuhusu chombo hiki ambacho ni kigeni kwa nchi yetu, nakuhakikisha kuwa Bodi uliyoiteua kusimamia Tume hii itahakikisha chombo hicho kinafanya kazi zake kwa weledi mkubwa.
#Nakuahidi kuwa Tume hii itahakikisha inalinda, inasimamia taarifa binafsi na kuhakikisha kwamba kazi hii inafanyika kwa weledi mkubwa.
*Aliyosema Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Emmanuel Mkilia*
#Nakushukuru Rais Samia kwa kutekeleza kwa vitendo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotaka haki ya faragha kwa kila Mtanzania, umewashika mkono Watanzania kwa kuwaletea sehemu ya kufikisha malalamiko yao yanayohusu uvunjifu wa faragha zao.
#Hatua hii kubwa na ya kihistoria, itafungua milango ya ushirikiano katika ulimwengu wa uchumi wa kidiplomasia na kidijitali.
#Natumia fursa hii kuwaomba Watanzania hasa taasisi za umma na binafsi zinazofanya kazi ya kukusanya na kuchakata taarifa binafsi, kufanya usajili na kupata kibali cha kuendelea kukusanya au kuchakata taarifa hizo.
*Aliyosema Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila*
#Mara nyingi wawekezaji wanashindwa kuwekeza mitaji yao kwa kuhofia machafuko katika kipindi cha uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu, nakuhakikishia Rais Samia kuwa uchaguzi utakuwa imara na safi. Amani na utulivu itakuwa ndio kipaumbele chetu.
*IMEANDALIWA NA IDARA YA HABARI - MAELEZO*





