BANDA MEDIA BLOG

SAMIA KAMA KOCHA NA ANAVYOPANGA NA KUPANGUA KIKOSI CHAKE

 


Tafakuri Jadidi:

Samia Kama Kocha Na Anavyopanga Na Kupangua Kikosi Chake…(3)

“ Aah, Batilda, Mheshimiwa Balozi Batilda Burian nimekupeleka Tanga. Batilda, nadhani kwa ulivyo hivyo utakwenda nao vizuri sana. Wazir ( Kindamba) alikuwa anatumia maguvu sana, Mnyapara sana. Sasa wewe nadhani utaendana nao. 

Usikubali wakuendeshe lakini usibishane nao. Nenda kasimame nao vizuri.” - Samia Suluhu Hassan.

Hili la Batilda limenikumbusha Mwalimu Nyerere alivyompeleka Marehemu Suleiman Kissoky kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa miaka ya 1970. Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa, Marehemu Dr. Kleruu hakuendana na wenyeji. Ikafikia hata akauawa kwa kupigwa risasi na mkulima Said Mwamwindi.

Suleiman Kissoky, kada wa TANU ambaye hakufika hata kiwango cha elimu ya Sekondari, ndiye aliyemudu kuwaongoza Wahehe. Aliweza ‘ Kwenda nao’.

Na hata zama za Mwalimu, kulikuwa na viongozi wenye sifa za kinyaparanyapara. Mwalimu naye aliwapeleka kule kunakohitaji staili ya  uongozi ya ‘ Kinyaparanyapara’ kulingana na mazingira ya maeneo hayo. Nchi hii kuna maeneo ambayo kiongozi mbabe mbabe hawezi kuyaongoza.

Naam, kwa sisi watu wa mpira, Rais wa Jamhuri tunaweza kumtafakari kama kocha wa mpira.

Kwa Rais Samia, yeye si kocha wa klabu. Amebeba dhamana ya  kuongoza ‘ Timu ya Taifa’.

Kama ilivyo kwa kocha wa mpira, naye hubeba maono na mfumo wa timu ili kuipeleka kwenye ushindi. 

Rais wa nchi naye ni mbeba maono na mfumo ikiwamo itikadi ya Chama chake. Ndiye msimamizi mkuu wa utekelezaji wa Ilani  ya Chama chake.

Kwenye soka, timu ikivurunda, kuna vidole vinaelekezwa kwa kocha. Kuna hata watakaotoa sauti na mashinikizo ya kutaka kocha aachie ngazi.

Kocha wa mpira anapaswa awe na ‘ Jicho la Mchezaji’. Kwamba awe na jicho la kumwona mchezaji ambaye akimwingiza kwenye kikosi anaweza kuwa na mchango kwenye kikosi kizima.  

Hivyo, kuwa na mchezaji ndani ya timu na sio mchezaji kwenye timu. Kuna tofauti kwenye mawili hayo. Kuna ambao hawaichezei timu bali wanacheza kwenye timu. 

Anayeichezea timu anajitoa kwa timu kwa kushirikiana na wenzake. Lakini, kuna ambao wanacheza peke yao na wanataka waonekane wao tu.

Kazi ya kocha, kama ilivyo kwa Kiongozi wa Siasa, ni kutafuta ‘ team players.’ 

Ndio maana, kwenye soka, mechi ikiendelea utamwona kocha muda wote ametulia akifuatilia mchezo. Kuna vitu ataonekana akiviandika hapa na pale ili avifanyie  kazi kabla ya kwenda mapumziko, wakati wa mapumziko na hata kipindi cha pili kikiendelea.

Kocha pia huwa na wasaidizi wake wa karibu kwenye benchi la ufundi. Mathalan, ndiye yule msaidizi utakayemwona akifungua ukurasa baada ya mwingine kwenye kitabu chake. Anafanya kazi ya kusoma mpango wa mchezo kwa jinsi walivyochora na nini cha kumshauri kocha. 

Mwingine ana kazi ya akinong’onezwa fulani atatolewa na fulani ataingia uwanjani, basi, huyo msaidizi wa kocha kazi yake ni kumwinua mchezaji husika na kumwamuru aanze kupasha.

Halafu,  kuna yule msaidizi muhimu wa kocha ambaye huenda kwenye mstari kabisa wa uwanja ili kufikisha kwa sauti maelekezo ya kocha mkuu kwa wachezaji. 

Utamwona wakati mwingine akiwafokea wachezaji mpaka sauti kumkauka;

“ Wewee, panda kulia na peleka mashambulizi katikati! Wewee beki tatu shuka chini na mwangalie adui huyo anapitia kulia…!

Naam, kuna mwenye kumsaidia kocha mkuu kwa jukumu hilo hata wakati mwingine anagombana na washika vibendera kwa kuambiwa anavuka mstari na kuingia uwanjani. Kwenye kutekeleza jukumu lake msaidizi huyo hapaswi kuogopa lawama ikiwamo matusi ya washabiki wa timu pinzani.

Kwa Rais Samia kama kocha hapo kuna wasaidizi wa Kocha Samia aina ya Majaliwa, Mpango, Makonda na wengine. Siku zote, mpango mkuu wa kocha ni kufanikisha ushindi wa timu kwa kuwatumia wasaidizi wake na wachezaji aliowateua kuingia kikosini. 

Na ilivyo, Rais Samia kama kocha ana kikosi kipana. Ndio maana ya panga- pangua yake ya kikosi haikosi wa kuwaingiza au kuwabadilisha namba kulingana na anavyousoma mchezo.

Oh! Samia kama kocha pia ameshaona mchezo utakavyokuwa mgumu kwenye baadhi ya maeneo uwanjani kama asipotafuta wachezaji sahihi wa kucheza nafasi hizo.

Mathalan, kuna hili la mabadililko ya tabia nchi na mazingira kwa ujumla wake.

“ Christina ( Mndeme) nakupeleka ukawe Naibu Katibu Mkuu ( Mazingira), katusaidie kwenye maeneo hayo. Kuna project ya green cooking kwa wanawake wa Afrika. Lazima tuanze na hapa nyumbani. Kanisaidie kwenye green cooking. Target yangu ikifika 20-30, wanawake asilimia 88 wawe wanapikia kwenye nishati safi. Kaisimamie ajenda ya green cooking na mazingira kwa ujumla.”- Samia Suluhu Hassan.

Hilo si jukumu dogo kwa aliyepewa akalisimamie. Ni ajenda muhimu yenye tija nyingi kijamii, kiuchumi na kimazingira. Inahitaji andiko jingine kuifafanua.

Ni Tafakuri Jadidi. Ya

Maggid Mjengwa.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG