*Aliyosema Mhe. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa*
#Hafla ya leo ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe za muungano, lengo lake mahsusi ni kushuhudia uzinduzi wa nembo na kauli mbiu kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 60 ya muungano.
#Nawapongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kwa uongozi wao makini ambao umekuwa chachu ya kudumisha muungano wetu. Watanzania wote wameendelea kuulinda na kuuheshimu muungano wetu ambao umeendelea kukuza udugu miongoni mwetu.
#Watanzania tuna kila sababu ya kujivunia muungano wetu kutimiza umri wa miaka 60. Ni ukweli usiopingika kwamba muungano wetu umeendelea kuwa na tija kubwa na kuchagiza maendeleo ya nchi yetu na wananchi wote kwa ujumla.
#Muungano wetu umefanya Tanzania liwe Taifa lenye utulivu, mshikamano, nguvu na mfano kwa mataifa mengi barani Afrika na duniani kwa ujumla.
#Natoa rai kwa Watanzania wote kuendelea kumwomba Mwenyezi Mungu aendelee kutujalia amani, utulivu na mshikamano, ili muungano wetu uweze kuendelea kudumu na kuimarika zaidi kwa manufaa ya vizazi vyetu.
*Maadhimisho ya mwaka huu yamepambwa na matukio mengine muhimu kama ifuatavyo:*
#Kutakuwa na uzinduzi wa sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya muungano utakaofanyika Zanzibar tarehe 14 Aprili, 2024 pamoja na uzinduzi wa maonesho ya biashara ya taasisi za muungano. Mgeni rasmi katika matukio hayo ni Mheshimiwa Dkt, Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
#Kutakuwa na maonesho ya muungano kwa upande wa Tanzania Bara yatakayofanyika Katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Jijini Dar es Salaam. Mheshimiwa Hemed Abdulla, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar atakuwa mgeni rasmi.
#Maadhimisho haya yataambatana na uzinduzi wa miradi ya maendeleo utakaoanza tarehe 15 Aprili na kuendelea hadi mwisho wa Mei, 2024.
#Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ataliongoza Taifa katika siku maalum ya maombi na dua kwa Taifa itakayofanyika katika uwanja wa Jamhuri, Dodoma tarehe 22 Aprili, 2024. Viongozi wa kitaifa wa dini zote watahudhuria katika ibada hiyo.
#Aidha, wilaya zote hapa nchini zitaandaa maombi kwa Taifa yatakayofanyika katika siku hiyo. Nisisitize kila Mkuu wa Wilaya aanze kufanya uratibu, ili nchi yetu yote ishiriki katika maombi na dua hizo.
#Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ataliongoza Taifa katika kuzindua kitabu cha historia ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Ikulu Dar es Salaam, shughuli itakayofanyika 23 Aprili, 2024.
#Tarehe 24 Aprili, 2024, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atatunuku nishani za Taifa kwa watu mbalimbali, shughuli hiyo itakafanyika Ikulu, Jijini Dar es Salaam.
#Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, Naibu Waziri Mkuu, atakuwa mgeni rasmi katika tamashala muungano litakalofanyika katika viwanja vya Tanganyika Packers, Jijini Dar es Salaam tarehe 25 Aprili, 2024.
#Mnamo tarehe 26 Aprili, 2024, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ataliongoza Taifa katika kilele cha maadhimisho ya sherehe za miaka 60 ya muungano yatakayofanyika katika Uwanja wa Uhuru, Jijini Dar es Salaam.
#Tarehe 14 Oktoba, 2024, siku ya kumbukizi ya Baba wa Taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bendera ya Taifa na Mwenge wa Uhuru vitapandishwa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro baada ya kuhitimisha mbio zake mkoani Mwanza.
#Mwenge huo pamoja na bendera vitafikishwa katika kilele cha mlima Kilimanjaro tarehe 19 Oktoba, 2024 saa 12.30 asubuhi.
#Ninapenda kuwafahamisha kuwa, maadhimisho ya miaka 60 ya muungano yamebeba kaulimbiu isemayo, Miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tumeshikamana na Tumeimarika, kwa Maendeleo ya Taifa Letu.
#Kauli mbiu hii thabiti, inatokana na ukweli kwamba tangu kuanzishwa kwa muungano mwaka 1964, Watanzania tumeendelea kuonesha mshikamano wa hali ya juu ambao umekuwa chachu ya maendeleo ya Taifa letu na wananchi wa pande zote mbili za muungano wameendelea kuwa imara katika kuhakikisha misingi ya kuasisiwa Taifa letu inazidi kuimarika.
#Kaulimbiu hii inatukumbusha kuwa, muungano wetu umekuwa kichocheo cha maendeleo kwa pande zote mbili za muungano. Hakuna mwananchi ambaye hajafikiwa na faida za muungano wetu.
#Watanzania wote, bara na visiwani tuendelee kuulinda, kuuenzi, kujivunia na kuuthamini muungano wetu. Muungano huu ni tunu adimu na adhimu inayopaswa kulindwa kwa gharama yoyote.
#Nitoe wito kwa wananchi wote wa pande mbili za muungano jitokezeni kwa wingi ili kushuhudia maadhimisho ya miaka 60 ya muungano pamoja na matukio yote kama yalivyoainishwa katika ratiba ya maadhimisho.
#Wananchi wote tumieni maadhimisho haya kutafakari tumetoka wapi, tuko wapi na tunaelekea wapi tangu muungano uliopoasisiwa mwaka 1964. Kaulimbiu ya maadhimisho haya ituongoze katika tafakuri hiyo ili kwa pamoja, Watanzania wote tuendelee kuulinda na kuutetea muungano wetu.
#Televisheni zetu zimeandaa makala maalum kuhusu mafanikio ya miaka 60 ya muungano kwa pande zote mbili, nitoe rai kwa wananchi wote kutenga muda wa kufuatilia vipindi hivyo, ili muweze kufahamu kwa undani kuhusu tija iliyopo katika muungano wetu.
#Taasisi zinazotoa elimu, ziendelee kufundisha mada kuhusu muungano wetu kuanzia elimu ya awali, ili watoto na vijana wetu waufahamu na wawe walinzi na hatimaye wawe vinara katika kuundeleza muungano wetu.
#Nchi yetu itaendesha uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa mwaka 2024, nitoe rai kwa wapiga kura wote kuhakikisha wanajiridhisha na kushiriki taratibu za kuwafanya kuwa na sifa za kushiriki kuchagua viongozi wenye uwezo na wenye nia njema na muungano wetu.
#Ninawasihi sana wananchi wote kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa. Huu ni uchaguzi muhimu kwani viongozi wa serikali za mitaa wanatakiwa wawe msingi imara wa maendeleo yetu, tuwachague wale wanaotosha, ili wasaidie kuharakisha maendeleo yetu.
*Aliyosema Mhe. Waziri wa Nchi - Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama.*
#Katika miaka 60 ya muungano wetu, Jamhuri ya muungano wa Tanzania inaongozwa na Rais wa kwanza mwanamke, ni jambo la kujivunia kwani sio tu tunaongozwa na Rais mwanamke, lakini ni mwanamke mbobezi, mwenye uwezo wa hali ya juu na aliyeuthibitishia ulimwengu mzima kwamba utendaji kazi wake umetukuka kwa viwango ambavyo havina mfano.
#Mwaka huu tunajivunia kwa kutimiza miaka 60 ya muungano wetu. Zipo sababu nyingi za kihistoria, kijiografia, kitamaduni, kibiashara, kisiasa na kiusalama ambazo wakati wote wa muungano wetu zimeendelea kutuunganisha kama Taifa moja la Tanzania.
#Sote tunafahamu uzito wa maadhimisho ya miaka 60 ya tukio lolote lile. Hivyo, hatuna budi kukaa pamoja kama Taifa moja kumshukuru Mungu na kuiadhimisha siku hii kwa furaha kubwa.
#Sherehe za kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya muungano, zitazinduliwa rasmi na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi tarehe 14 Aprili, 2024 katika uwanja wa Maisara, Zanzibar. Tukio hili litafuatiwa na uzinduzi wa miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.
*Aliyosema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo*
#Nakuhakikishia Mhe. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, kuwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Watanzania wanayafahamu yale yote ambayo walipaswa kujivunia kupitia muungano huu.
#Namshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa usimamizi wao unaofanikisha twende kifua mbele katika miaka 60 ya muungano wetu.
#Leo tunapoanza safari hii, tunawashukuru viongozi wetu wakuu kwa kutuheshimisha sana kwa sababu katika kipindi chao cha miaka mitatu wameweza kutatua kero 15 za muungano kati ya kero 18 zilizokuwa zimebakia.
*Aliyosema Mhe. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (Sera, Uratibu na Baraza la Uwakilishi), Hamza Hassan Juma*
#Sisi Watanzania, muungano huu ni tunu yetu kubwa, hivyo tuna wajibu wa kuulinda, kuutunza na kuutetea kwa hali zote. Kuhakikisha kuwa unaendelea kudumu ili wananchi waendelee kuishi kwa usalama na amani na tuwaenzi viongozi waasisi wa muungano huu.
#Tukio hili la uzinduzi wa nembo na kauli mbiu ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, linaenzi mawazo ya viongozi waasisi wa muungano wetu.
#Muungano huu kudumu kwa miaka 60 sio jambo jepesi, tayari kuna misukosuko mingi ambayo muungano huu umepitia, mathalan kwenye Bunge la Katiba, kuna watu waliukana muungano kuwa haupo kwa sababu hakuna hati ya muungano. Katika kitu ambacho ni tunu, ni hati ya muungano ambayo ipo na imehifadhiwa.
#Zanzibar tuko tayari kwa ajili ya kutekeleza yatakayoelekezwa katika shughuli hii.
*Aliyosema Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule*
#Naungana na Watanzania wengine kuendelea kuwapongeza viongozi wetu wakuu kwa kuendeleza muungano wetu ambao una historia ya muda mrefu na kuendelea kuimarisha na kuufanya muungano kuendelea kuwa imara.
#Nawapongeza pia Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa kuendelea kuratibu Muungano huu katika utulivu na amani na kufanya nchi hizi mbili zikiendelea kuimarika kwa mshikamano mkubwa.
*IMEANDALIWA NA IDARA YA HABARI - MAELEZO*

