.......................
NA JOHN BANDA, DODOMA
SERIKALI Imewahakikishia Watanzania kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa utazingatia "4 R" ili kila chama kipate nafasi sawa.
Hikisho hilo limetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dk.Festo Dugange jijini Dodoma, wakati akifungua kikao cha kupitia rasimu za kanuni za uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa unao tarajia kufanyika mwaka huu.
“Uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024 utazingatia maono ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kama ambavyo tumesikia katika majukwaa mbalimbali akisisitiza “Four R” kwa maana ya Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya,”alisema.
Aliongeza kuwa;”Hivyo, uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika mwaka huu utazingatia maono hayo ili kila chama kipate nafasi sawa katika uchaguzi,”.
Dk.Dugange alizitaja rasimu za kanuni zilizoandaliwa kuwa ni Rasimu ya Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Wilaya za Mwaka, 2024.
Alitaja rasimu nyingine kuwa ni uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mtaa na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa katika Mamlaka za Miji za Mwaka, 2024 na uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji za Mwaka, 2024.
Katika hatua nyingine alisema Rasimu nyingine iliyoandaliwa ni mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji Midogo za Mwaka, 2024.
“Hivyo, mmealikwa kwa ajili ya kupitia rasimu za Kanuni zilizoandaliwa na kutoa maoni yenu kwa lengo la kuboresha. Ni matumaini yangu kuwa kila mmoja wenu atashiriki kikamilifu na kutumia muda vizuri katika kutoa michango chanya itakayosaidia kuboresha rasimu zilizoandaliwa,”alisema.
Kwa Upande wake Sheikh Hemed Mwakindege amesema kikao hicho ni muhimu kwasababu kinakusanya viongozi wa dini ambao ni wadau muhimu wa kuhubiri amani, mshikamano na upendo.
“Tunamshukuru Rais Dk.Samia kwa dhamira yake ya kushirikisha viongozi wa dini ambapo ni ishara kubwa ya nia njema ya kutenda demokrasia katika ardhi ya Tanzania na ishara ya uchaguzi wa serikali za mitaa kuwa wa haki na huru kwa asilimia zote,”amesema
Naye Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania, Askofu Dk.Israel Gabriel amesema vongozi wa Dini wamekaa kama wawakilishi wa neema za mwenyezi mungu duniani.
“Maelezo ya serikali yanaonyesha ni kwa namna gani imefanya maandalizi katika uchaguzi wa serikali za mitaa. Naomba viongozi wengine wa serikali muendelee kuunga mkono jitihada za Rais Dk.Samia za kuhamasisha ushrikishaji.
Ameongeza kuwa“Niwasihi wagombea kuepuka siasa za matusi na rushwa kwasababu kuna maisha baada ya uchaguzi na wagombea wajiandae kuwa katika uchaguzi kuna kushinda na kushindwa kwahiyo wajiandae kisaikolojia,”alifafanua