...............
Na Mwandishi wetu. Sabasaba Dar.
MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeanza kutekeleza zoezi la kuchapisha upya vitambulisho vilivyochapishwa chini ya ubora na kugaiwa kwa wananchi.
Akizungumza juu ya zoezi hilo jana Jijini Dar es Salaam wakati wa mahojiano kwenye Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa, 'Sabasaba', Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Geofrey Tengeneza amesema wamekuwa wakipokea malalamiko kutoka kwa Wananchi wa Mikoa mbalimbali kuhusu ubora hafifu wa baadhi ya Vitambulisho hivyo.
"Tumekuwa tukipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya Wananchi wa Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro Dar es Salaam na mingine kuwa vitambulisho walivyopewa vimefutika picha, na majina," alisema.
Baada ya kufanya utafiti na kubaini ukweli juu ya kuwepo kwa changamoto hiyo, Tengeneza amesema NIDA imeamua kuzindua zoezi maalumu ya kuvikusanya vitambulisho hivyo kutoka kwa Wananchi ili kuvichapisha upya.
"Napenda kuchukua nafasi hii kuujulisha umma wa Watanzania kwamba Mwananchi yoyote mwenye kitambulisho kilichofutika picha na maandishi akirejeshe kwenye ofisi za kata yake, au ofisi za NIDA zilizopo karibu nae ili achapishiwe na kupowa kitambulisho kipya ndani ya muda mfupi," alisema.
Amesema Mamlaka imejipanga kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa weledi na ubora ili kuhakikisha Wananchi husika wanapata vitambulisho vyao ndani ya muda wa wiki mbili pekee.
"Ili kwenda na kasi kubwa ya uhitaji wa vitambulisho vya Taifa kwa Wananchi hapa nchini tulilazimika kuchapisha vitambulisho vingi sana ndani ya muda mfupi, zoezi kubwa ambalo lilisababisha baadhi ya Vitambulisho kuchapishwa chini ya kiwango kinachotakiwa," Tengeneza alieleza.
Amesema mpaka sasa, Mamlaka imefanikiwa kuchapisha na kutoka vitambulisho kwa asilimia kubwa sana ya Watanzania, na kazi bado inaendelea kuwafikia Wananchi wachache waliosalia.
"Kimsingi, Takwimu zetu zinaonyesha kuwa kila Mtanzania aliyeomba kupatiwa kitambulisho Cha Uraia na aliyekidhi vigezo vilivyowekwa na Serikali ameshachapishiwa kitambulisho chake," alieleza.
"Changamoto iliyopo hivi sasa ni kwamba watu wengi, hususan Mijini hawajaenda kuchukua vitambulisho vyao, hali ambayo inasababisha msongamano wa vitambulisho kwenye vituo," alisema.
MWISHO....



