BANDA MEDIA BLOG

TAKUKURU YAWAPIGA MSASA WANAHABARI MADHARA YA RUSHWA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA

 


Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza, James Ruge akisisitiza jambo kwa wakandishi wa habari (hawapo pichani),leo alipofungua mafunzo ya kuwajengea uwezo kuhusu rushwa katika uchaguzi.

Mkuu wa Dawati la Elimu TAKUKURU,Maua Ali akifafanua jambo wakati wa mafunzo ya waandishi wa habari leo.
Eli Makalla akiwasilisha mada ya ushiriki wa vyombo vya habari katika mapambano dhidi ya rushwa leo.
Waandishi wa habari wakimsikiliza Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Misungwi, Eli Makalla wakati kifafanua jambo kuhusu rushwa katik uchaguzi.
Mkuu wa Dawati la Uchunguzi TAKUKURU mkoani Mwanza, Stella Bukulu, leo akiwaeleza waandishi wa habari namna wanavyochunguza  miradi ya maendeleo.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza,James Ruge, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani),leo wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo.Picha na Baltazar Mashaka.
………
NA BALTAZAR MASHAKA,MWANZA
MKUU wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza,James Ruge amesema watawatumia waandishi wa habari kuelimisha wananchi madhara ya rushwa katika uchaguzi,kwa sababu wanaaminika,wana nguvu na nafasi ya kuifikia jamii kupitia taarifa mbalimbali.

Akifungua kikao kazi cha siku moja cha kuwajengea uwezo waandishi wa habari mkoani humu,leo amesema kwa mujibu wa sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa,lengo ni kukuza na kuhamasisha misingi utawala bora na kutokomeza rushwa nchini,kwa kuzuia na kushirikisha umma kwa njia ya elimu.

“Tuko hapa kujengeana uwezo wenye lengo la kuongeza ujuzi na ufanisi katika kuelimisha jamii ubaya wa rushwa katika mapambano dhidi ya rushwa,tunapoelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani mwakani,tuangalie namna gani tutazuia na kupambana na rushwa katika uchaguzi,”amesema Ruge.

Amesema mafunzo hayo yenye mada ya nafasi ya vyombo vya habari katika mapambano dhidi ya rushwa,ni maandalizi ya uchaguzi wa mwaka huu wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu 2025.

Amesistiza katika kuhakikisha wananchi wanashiriki vyema uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu,watavitumia vyombo vya habari na waandishi wa habari kuwaelimisha.

Kwa mujibu wa Ruge waandishi wa habari ni kalamu ya dhahabu, wanaaminika katika jamii,wana na nafasi ya kuifikia kupitia taarifa mbalimbali,hivyo TAKUKURU itaendea kuwatumia kufikisha elimu wananchi watambue ubaya na madhara ya rushwa.

“TAKUKURU inatambua waandishi na vyombo vya habari vinaaminika katika kuhakikisha taarifa au habari inafikia wananchi kwa ustawi wa jamii kwa kutumia kalamu zao kwa weledi,”amesema Ruge.

Mkuu huyo wa TAKUKURU mkoani humu amesisitiza mafunzo hayo  yataongeza ujuzi na ufanisi wa kuelimisha jamii ubaya wa rushwa na kuhamasisha wananchi kushiriki mapambano dhidi ya rushwa kwa kuzuia,kukemea na kutoa taarifa za vitendo hivyo.

Kwa upande wake Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Misungwi, Eli Makalla akiwasilisha mada ya nafasi ya vyombo vya habari katika mapambano dhidi ya rushwa amesema kifungu cha 7(b)kikisomwa pamoja na kifungu cha 45 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( Sura ya 329) kinaitaka TAKUKURU ihamasishe ushiriki wa wadau katika kuondoa rushwa nchini.

“Tunapoelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani,tunaamini tutasaidiana kuwaelimisha wananchi madhara ya vitendo vya rushwa katika jamii na uchaguzi,ni adui wa haki,inakwamisha maendeleo na ni miongoni mwa maadui ujinga,maradhi na umasikini,”amesema.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC),Edwin Soko ameishauri TAKUKURU kuwalinda waandishi wanaotoa taarifa za vitendo vya rushwa huku ikiwatahadharisha kujiepusha na vishawishi vya rushwa wakati wa uchaguzi.

Amesema nchi inapoelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa wandishi wa habari wasikubali kutumika kwa rushwa ndogo ndogo na kuiomba TAKUKURU iwalinde wanaoibua ama kutoa taarifa ya vitendo vya rushwa.

“Tunayo dhamana kubwa ya kushiriki vita dhidi ya rushwa tusiishie kuhoji TAKUKURU inafanya nini,tukosoe kwa kujenga tukiangalia uwezo na mzigo ilioubeba,bajeti,rasilimali watu na vitendea kazi vilivyopo kama tunataka kupata maendeleo na kujenga jamii salama isiyo na rushwa,”amesema.

Ameiomba taasisi hiyo kuhakikisha inawalinda wanahabari wanaofichua vitendo vya rushwa katika chaguzi na ipo mifano baadhi wamekuwa wakibambikwa kesi wanapofuatilia habari  za rushwa

Aidha taasisi hiyo mkoani imepanga kukutana na wadau mbalimbali kutoa elimu ya madhara ya rushwa katika uchaguzi ikianza na waandishi wa habari mkoni humu

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG