Baadhi ya akina mama waliopata kazi katika Shamba la miti Mpepo wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma,wakimwagilia maji bustani ya miche ya miti inayooteshwa kabla ya kupandwa kwenye mashamba yanayomilikiwa na wakala wa misitu Tanzania(TFS).

Wafanyakazi wa shamba la miti Mpepo kata ya Mpepo Halmashauri ya wilaya Nyasa mkoani Ruvuma,wakiweka udongo kwenye viliba kabla ya kuweka mbegu za miti inayooteshwa katika shamba la miti Mpepo wilayani Nyasa,kulia ni Mhifadhi misitu mwandamizi wa TFS John Kimolo.
Na Mwandishi Maalum,
Nyasa
WAKALA wa huduma za misitu Tanzania(TFS),umewataka wananchi hususani wanaojishughulisha na kilimo kuacha kutumia moto kama njia ya kusafisha mashamba yao.
Badala yake wameshauriwa kutumia mbinu mbadala ikiwemo majembe na zana nyingine ili kuepusha uharibifu wa mazingira unaoweza kusababisha majanga ya moto katika misitu na uoto wa asili.
Wito huo umetolewa na Mhifadhi misitu mwandamizi wa TFS John Kimolo, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari waliotembelea shamba la miti Mpepo kata ya Mpepo wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.
Alisema,wakulima wanapotaka kuandaa na kusafisha mashamba yao wanapaswa kuchukua tahadhari na kupata ushauri wa kitaalamu ili kuepuka kutokea kwa majanga ya moto katika misitu ya asili na miti ya kupandwa na maeneo ya uoto wa asili.
“wananchi wanapoandaa mashamba yao wanatakiwa kufyeka nyasi na miti na kukusanya mabiwi na wachome kwa kuzingatia mwelekeo wa upepo,sisi kama shamba la miti Mpepo tutaendelea kutoa elimu juu ya kuzingatia utumiaji sahihi wa moto kwenye mashamba”alisema Kimolo.
Alisema,kwa muda mrefu wananchi wa kata ya Mpepo wamekuwa na utamaduni wa kusafisha mashamba kwa kuchoma moto njia ambayo siyo sahihi na haina nafasi tena kwani inasababisha majanga makubwa ya moto kwenye maeneo mbalimbali yaliyohifadhiwa.
Aidha alisema,Shamba la miti Mpepo limeanzisha bustani ya miti ambayo inapandwa kwenye mashamba ya Serikali,taasisi za Serikali na kugawa miche ya miti kwa watu binafsi ili waweze kupande katika maeneo yao kwa ajili ya kujiongezea kipato.
Alisema,katika bustani hiyo wafanyakazi wengi ni wanawake kwa sababu wanawake ni watu wanafanya kazi zao kwa umakini mkubwa na hata wakipewa maelekezo wanapokea maelekezo haraka ikilinganisha na wanaume ambao hawafanyi kazi hizo vizuri.
Alieleza kuwa,kazi ya kuotesha miche ya miti ni ngumu inayohitaji kukaa na kuinama muda mrefu ambayo ni rahisi kwa wanawake kumudu kutokana na asili yao tofauti na wanaume ambao wanashindwa kufanya kazi hiyo.
Kwa mujibu wa Kimolo,katika bustani hiyo miche ya miti inayooteshwa ni jamii ya misindano inayopandwa mahususi kwenye mashamba yaliyopo safu za Mpepo,Kivulungwa na Lusewa ambazo zinastawi vizuri miti.
Alisema,safu na Liuli zilizopo pembezoni mwa ziwa Nyasa imepandwa miti ya aina ya misaji(tiki)inayostawi vizuri kwenye ukanda wa chini.
Diwani wa kata ya Mpepo Anderson Haule alisema,tangu Serikali kupitia wakala wa huduma za misitu Tanzania(TFS)ilipoanzisha mradi wa upandaji miti umesaidia wananchi wa kata hiyo kupata ajira za muda na wengine ajira za kudumu na hivyo kupunguza tatizo la ajira hasa kwa vijana na wanawake.
Aidha alisema,wananchi wameanza kupanda miti ya kibiashara ambayo imewawezesha kujipatia kipato badala ya kutegemea kilimo cha zao la mahindi ambalo lina changamoto kubwa ya soko la mahitaji makubwa wakati wa maandalizi yake.
Mkazi wa kijiji cha Mpepo Happy Nchimbi,ameishukuru TFS kwa kuleta mradi wa bustani ya miti kwani umewasaidia watu wengi hususani wanawake kupata ajira inayowaletea kipato tofauti na hapo awali ambapo walitegemea kupata fedha baada ya kuuza mazao.
Anna Ndunguru,ameipongeza TFS kwa kuwajali wananchi wa kata ya Mpepo kutokana na kutoa ajira mbalimbali zilizopunguza muda mwingi kwa vijana kukaa vijiweni.
