BANDA MEDIA BLOG

WANANCHI WAKUBALI YAISHE, BANGI KUBAKI HISTORIA TARIME

 





NA MWANDISHI WTU, TARIME

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama ikiwemo jeshi la polisi, jeshi la akiba pamoja na wananchi imefanya operesheni kubwa ya kihistoria kwa muda wa wiki tatu katika wilaya ya Tarime na Serengeti, mkoani Mara kwa lengo la kukabiliana na tatizo la uzalishaji na usambazaji wa dawa za kulevya, hususan bangi.

Operesheni hiyo imefanyika katika vijiji vya  Matongo, Nyarwana, na Weigita vilivyopo bonde la Masinki, pia vijiji vya  Nkerege, Kembwe, Nyakunguru na Iseresere pamoja na eneo la bonde la mto Mara. 

Akizungumza mara baada ya operesheni hiyo tarehe 8 Oktoba, 2024 Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema, jumla ya ekari 3,007.5 za mashamba ya  bangi  zimeteketezwa katika operesheni hiyo. Aidha, kilogramu 7,832.5  za bangi kavu, na kilogramu 452 za mbegu za bangi  zilikamatwa, ambapo watuhumiwa 17 walikamatwa na tayari wamefikishwa mahakamani.

Kamishna Lyimo amesema operesheni hii ni sehemu ya jitihada za serikali kulinda jamii dhidi ya madhara ya dawa za kulevya na amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kutoka kwa wananchi katika kutoa taarifa kuhusu shughuli zinazohusiana na dawa hizo.

Mamlaka imebaini kuwa, kilimo cha bangi mkoani Mara kinafadhiliwa na raia wa nchi jirani ambao huwapa mitaji wakulima wa Tarime kisha bangi ikishakomaa huvunwa na kusafirishwa kwenda  kuuzwa. 

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG