Lord Carrington, kutokana na misimamo na jeuri ya Mugabe, hata wakati huo, alimwezea Mugabe kama mjusi ( reptillian).
Na tabia za mjusi ni pamoja na kuwa na damu baridi na ngozi ngumu.
Ikumbukwe, katika miaka yake kumi ya mwanzo kama Kiongozi Mkuu wa Zimbabwe, Robert Mugabe alkuwa kipenzi cha mataifa ya Magharibi. Sera zake za Elimu, Afya na Ustawi wa Jamii zilipigiwa mfano hata na wakubwa wa Magharibi.
Mugabe alikuwa akifanya kazi ofisini kwa saa 16. Lakini, ahadi kuu ya ukombozi wa Zimbabwe iliyowekwa na ZANU kwa watu wa Zimbabwe ilikuwa ni ARDHI, kwa maana ya Wazimbabwe kupata matunda ya Uhuru kupitia kugawiwa ardhi pia.
Lakini, ahadi hii utekelezaji wake ulitegemea fadhila za utawala wa Kihafidhina wa Uingereza ( Margreth Thatcher) ulioahidi kutoa fedha za kugharamia fidia.
Ahadi hii haikutekelezwa kama ilivyopaswa na ikawa chanzo cha mgogoro mkubwa na ugomvi wa Mugabe na mawaziri wakuu waliofuatia wa Uingereza baada ya Magreth Thatcher.
Akina Tonny Blair na hata Gordon Brown hawakutekeleza kilichoahidiwa kwa visingizio mbali mbali. Huku nyumbani Robert Mugabe akawa anabanwa na Wazimbabwe wakiwemo maveterani wa Chimurenga.
Ndipo sera za Mugabe za ' indigenisation of the economy' ikiwa na maana ya kunyang'anya ardhi kwa nguvu zikaanza huku akigombana zaidi na wakubwa. Kukawa na vitisho vya wenye mashamba - Wazungu kumpeleka Mugabe mahakamani.
Mugabe akawajibu;
" I, Robert Mugabe, cannot be dragged to court by a settler."
Kwamba Robert Mugabe mimi, kamwe siwezi kufikishwa mahakamani na setla.
Wakubwa wa Nchi za Magharibi walipodai kuwa Mugabe awalipe fidia aliowanyang'anya ardhi, naye Mugabe akaja na hoja, kwa kusema;
" How can these countries who have stolen land from the Red Indians, the Aborigines and the Eskimos dare to tell us what to do with our land.?"
Kwamba iweje hawa waliowaibia ardhi wenyeji wa asili Aborigine, Wahindi Wekundu na Waeskimo waje leo kutuambia nini cha kufanya na ardhi yetu?
Ikafika wakati, kwenye vita vya maneno, Mugabe alimwita Tony Blair kuwa ni ' Tony B-liar' akiwa na maana ni mwongo.
Naam, kama Emmerson Mnangagwa ni mamba, Robert Mugabe alikuwa mjusi. Wote ni wa jamii moja. Wana damu baridi na ngozi ngumu.
Maggid Mjengwa.
Tags
HISTORIA