Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MWENYEKITI wa kijiji cha Namalulu Wilayani Simanjiro, Mkoani Manyara, Marumai Kirikai amepumzishwa kazi kwa muda wa siku 28 ili kupisha uchunguzi wa matumizi mabaya ya madaraka katika kijiji hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Fakii Raphael Lulandala ameunda kamati ya watu saba itakayofanya uchunguzi kwa muda wa siku 24 na baada ya siku 28 endapo Mwenyekiti huyo atabainika hausiki na tuhuma hizo atarejea kwenye nafasi yake.
Lulandala ameyasema hayo wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Namalulu, baada ya kusikiliza kero, malalamiko na changamoto zao.
Ameeleza kwamba hamsimamishi kazi Mwenyekiti huyo ila anapisha uchunguzi kwa muda wa siku 28 na endapo hatakuwa na makosa atarejea tena kwenye nafasi hiyo.
“Hausimamishwi kaz ila unakaa pembeni kwa muda wa siku 28 ili kupisha uchunguzi na ofisa mtendaji wa kijiji cha Namalulu Sarafina Olotu ataongoza kijiji kwa kipindi hiki,” amesema DC Lulandala.
DC Lulandala amewataja wajumbe saba wa kamati hiyo ni ofisa ardhi wa halmashauri, afisa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) na ofisa wa ofisi ya DSO.
Amewataja wajumbe wengine ni ofisa mtendaji wa kata ya Naberera, askari polisi wa upelelezi na ofisa maendeleo ya jamii kata ya Naberera.
“Chunguzeni nyaraka zote, iteni watu wote wanaotuhumiwa kunyang’anya wenzao ardhi, anayemiliki eneo Namalulu afike kila atakayeitwa na kamati aje na huyo Mwenyekiti wa kitongoji aliyekataa shamba aitwe,” amesema DC Lulandala.
Amesema kamati hiyo ichunguze endapo kuna viashiria vya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka na ugawaji holela wa mashamba katika kijiji hicho.
“Chunguzeni bila kujali cheo cha mtu, dini au nafasi ya mtu na ofisa TAKUKURU, Dunia Mazigo ukikuta kuna jinai anza uchunguzi hapo hapo,” amesema DC Lulandala.
Mmoja kati ya wakazi wa kijiji hicho Mosses Malamia amesema Mwenyekiti wa kijiji hicho na baadhi ya wajumbe wa serikali ya kijiji walijigawia mashamba kila mmoja ekari 30 bila kufuata utaratibu.
“Mwenyekiti wa kijiji na wajumbe wake walikata shamba la shule na kujigawia ekari 30 kila mmoja ila Mwenyekiti wa kitongoji cha Ormot, alikataa kuchukua shamba,” amesema.
Hata hivyo, akizungumza kabla ya uamuzi huo, Mwenyekiti huyo Kirikai ameeleza kwamba ameongoza kijiji hicho kwa uadilifu kwa kipindi cha miaka 10.
“Mheshimiwa DC mimi niliomba kura mara moja tuu pale nilipochaguliwa kwa mara ya kwanza ila vipindi vingine nilikuwa ninawaeleza wanirudishe kama nimewaongoza vyema,” amesema.
Amesema hata shamba alilonalo amepata kihalali na hajachukua shamba la mtu kwa ubabe au kwa ubadhirifu wowote ule,” amesema Kirikai.
Amesema ameongoza na kufanikisha maendeleo mengi ikiwemo maji na shule kila kitongoji ila kuna baadhi ya watu wanachuki naye za kisiasa.
