NA MWANDISHI WETU, DODOMA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imeweka wazi kuwa haitavumilia tena tabia za kujiunganishia huduma ya maji bila kufuata sheria na taratibu rasmi. Aidha, mamlaka hiyo imetoa onyo kali kwa wananchi wote wanaojihusisha na vitendo vya kuingilia miundombinu ya maji kinyume cha sheria, ikisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wahujumu hao.
Onyo hilo limekuja kufuatia tukio lililotokea katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma ambapo DUWASA imeendesha ukaguzi wa miundombinu ya maji kwa lengo la kugundua na kukomesha vitendo vya wizi wa maji. Katika ukaguzi huo, mteja mmoja aliyejitambulisha kama Bw. Felix Maneno, mwenye yard iliyopo karibu na Chuo cha Ufundi Stadi VETA, alikamatwa akijihusisha na matumizi ya maji kinyume cha utaratibu.
Afisa Mapato wa DUWASA, Bw. Fridolin Henjewele, akizungumza na waandishi wa Habari Januari 28,2026 Jijini Dodoma,amesema kuwa “tumemkamata mteja huyu akitumia maji bila kufuata sheria na utaratibu wa DUWASA. Mkaguzi wetu aligundua kuwa mmiliki huyo ameingilia miundombinu kwa kuongeza laini ya maji bila idhini yoyote.”
Aidha, Mkaguzi wa Miundombinu ya Maji na Mtandao wa Maji Taka DUWASA, Bw. Alex Robert Makelemo, amebainisha kuwa Bw. Felix Maneno ni mteja wa muda mrefu wa DUWASA ambaye huduma yake ilisitishwa kutokana na deni lililokuwa limekusanywa. “Baada ya kusimamishwa huduma, alijaribu kuingilia miundombinu kwa kuchimba ukuta na kuingiza laini nyingine ya maji moja kwa moja kwenye tenki, alitumika kwa shughuli za kuosha magari na matumizi ya walinzi wake,” amesema Bw. Makelemo.
Ameongeza kuwa Bw. Maneno tayari amepatiwa taarifa kwa simu na kuombwa kufika ofisini kwa ajili ya majadiliano, ingawa mpaka sasa bado hajafika. DUWASA pia imemwandikia barua rasmi ya wito ili aelewe gharama na hatua zinazochukuliwa kwa mujibu wa sheria.
DUWASA imesisitiza kuwa itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa haki kwa wananchi wote na kuendelea kupambana na vitendo vya hujuma na wizi wa maji kwa kutumia sheria kwa nguvu zote.

