
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Asha Rose Migiro akizungumza na mabalozi wa mashina kutoka wilaya za Temeke na Kigamboni katika Kikaukazi kwenye ukumbi wa PTA Temeke Januari 07, 2026.
NA MWANDISHI WETU
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Asha Rose Migiro, amehimiza chama kuwatumia ipasavyo wazee na wastaafu waliolitumikia chama kwa muda mrefu katika kufundisha somo la itikadi kwa viongozi na wanachama vijana, akisema kundi hilo lina hazina kubwa ya historia, uzoefu na misingi ya chama.
Akizungumza na mabalozi wa mashina kutoka Wilaya za Kigamboni na Temeke katika kikao kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa PTA Temeke jijini Dar es Salaam Januari 07, 2026, Dkt. Migiro amesema wazee hao wanabeba kumbukumbu muhimu za safari ya CCM tangu kuanzishwa kwake, jambo linalowafanya kuwa walimu sahihi wa itikadi, uzalendo na maadili ya uongozi kwa kizazi kipya cha chama.
Amesema wazee na wastaafu wamekuwa wakijitokeza mara kwa mara katika shughuli za chama kwa hiari na uzalendo mkubwa, hivyo amehimiza kuwatumia kwa makusudi katika kutoa mafunzo ya itikadi ili kuimarisha misingi ya CCM na kuendeleza falsafa yake miongoni mwa viongozi na wanachama vijana.
Aidha, amebainisha kuwa CCM kina wapenzi na wakereketwa wengi ndani na nje ya chama, na njia ya kuendelea kuwavutia ni kuimarisha mahusiano ya karibu kati ya chama, wanachama na jamii kwa ujumla.
Ameeleza kuwa kura nyingi zilizopatikana katika chaguzi zilizopita hazikutokana na wanachama wa CCM pekee, bali pia Watanzania waliokuwa na imani na itikadi ya CCM pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi iliyonadiwa nchi nzima na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa Dkt. Migiro, imani hiyo ndiyo iliyowezesha CCM kurejea madarakani kwa kishindo, hivyo amehimiza viongozi na wanachama kuwa karibu na jamii na kutambua kuwa changamoto za wananchi ni sehemu ya wajibu wao wa uongozi.
Amebainisha kuwa mahusiano mazuri, ushirikiano na kauli njema kati ya chama, wanachama na jamii vitaendelea kuimarisha umoja wa kitaifa na kulifikisha taifa katika maendeleo endelevu.
Katika maelezo yake, amesema chama na Serikali katika Mkoa wa Dar es Salaam, hususan Wilaya za Temeke na Kigamboni, ni mhimili mmoja unaopaswa kushirikiana kwa karibu katika utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Amesisitiza kuwa jukumu la chama siyo kuishutumu Serikali, bali kuisimamia na kuikumbusha ahadi zake kwa wananchi kwa kutumia Ilani ya CCM kama nyenzo kuu ya uwajibikaji.
Aidha, amesema madiwani walipewa vijitabu vidogo vya Ilani wakati wa kampeni, ambavyo vinapaswa kusomwa sambamba na Ilani Kuu ili kusaidia kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika ngazi za halmashauri.
Dkt. Migiro amehimiza viongozi kushuka hadi ngazi za wilaya na halmashauri ili kufuatilia utekelezaji wa ahadi na kupata taarifa za mara kwa mara kupitia mifumo ya uwajibikaji ya chama na Serikali.
Amesema ni muhimu viongozi kuwaeleza wananchi yale yaliyotekelezwa, na pale wananchi wanapotoa maoni au hoja, kuyapokea na kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na viongozi wa chama na Serikali.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo amesema CCM kina vitega uchumi mbalimbali vinavyopaswa kufahamika, kusimamiwa na kuendeshwa kibiashara ili kukiimarisha chama kiuchumi.
Ameonya kuwa viongozi hawapaswi kuwa mstari wa mbele kuharibu miradi ya chama, bali wanapaswa kuisimamia ipate tija na kusaidia CCM kujitegemea kiuchumi.
Ameongeza kuwa uzoefu kutoka nchi rafiki unaonesha vyama vinavyojenga na kuimarisha vitega uchumi huwa imara zaidi, hali inayochangia ustawi wa chama na taifa kwa ujumla.
Dkt. Migiro amehitimisha kwa kusema kuwa katika uchaguzi uliopita, CCM iliendesha uchaguzi kwa kutumia fedha za ndani kutokana na uimara wa kiuchumi wa chama, hivyo amehimiza viongozi kuanzisha na kusimamia miradi ya kiuchumi katika maeneo yao ili kuendeleza dhana ya kujitegemea.







