
Na Silivia Amandius – Bukoba
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, Acton Rwankomezi, amewaagiza waratibu wa elimu katika kata zote za Manispaa hiyo kusimamia kikamilifu zoezi la upokeaji wa wanafunzi wa elimu ya awali, shule za msingi na kidato cha kwanza bila kuwepo kwa vikwazo vinavyoweza kuwanyima watoto haki yao ya msingi ya elimu.
Meya Rwankomezi ametoa agizo hilo wakati wa kikao chake na watumishi wa Kata ya Kagondo, ambapo amesisitiza kuwa hakuna mwanafunzi anayepaswa kuzuiwa kuripoti shuleni kwa sababu yoyote ile, ikiwemo kukosa sare za shule au mahitaji mengine yasiyo ya msingi kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali.
Amesema agizo hilo linatokana na maelekezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, ambaye amesisitiza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha watoto wote wanapata fursa sawa ya elimu bila ubaguzi wala vikwazo.
Meya Rwankomezi ameongeza kuwa waratibu wa elimu katika ngazi ya kata na wasimamizi wa shule wanapaswa kutekeleza maagizo hayo kwa uadilifu, uwajibikaji na kwa kuzingatia maslahi ya mtoto, akisisitiza kuwa elimu ni haki ya kila mtoto na si upendeleo.
Kwa upande wao, baadhi ya watumishi wa Kata ya Kagondo waliohudhuria kikao hicho wameahidi kuyatekeleza maelekezo hayo kwa vitendo kwa kuhakikisha wanafunzi wote wanaoripoti shuleni wanapokelewa mara moja na kuanza masomo bila usumbufu.
