BANDA MEDIA BLOG

WASTAAFU KAGERA WALALAMIKIA PENSHENI NDOGO,

 


Na Silivia Amandius

Kagera.

Wastaafu na wanachama wanaokaribia kustaafu katika Mkoa wa Kagera wameeleza changamoto wanazokumbana nazo baada ya kupokea mafao yao, wakisema kiwango cha pensheni wanachopata hakilingani na gharama halisi za maisha zinazozidi kupanda kila siku.

Baadhi yao wamesema fedha wanazopokea hazitoshelezi mahitaji ya msingi kama matibabu, chakula na malezi ya familia, hali inayowafanya kuendelea kuishi kwa wasiwasi hata baada ya kumaliza utumishi wao serikalini na katika sekta binafsi.

Akizungumza katika mafunzo yaliyoandaliwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika ukumbi wa KCU Bukoba Januari 29, mmoja wa wanufaika, Bi. Angelina Kokushubila, amesema mafao wanayopata ni madogo ukilinganisha na hali ya maisha ilivyo sasa. Ameomba NSSF kuendelea kuboresha viwango vya mafao ili kuhakikisha wastaafu wanaishi maisha yenye heshima na usalama wa kifedha badala ya kuendelea kuwa tegemezi au kuingia kwenye madeni.

Kwa upande wake, Meneja wa Huduma kwa Wateja wa NSSF Mkoa wa Kagera, Bw. Robert Cosmas Kadege, amesema changamoto kubwa iliyobainika ni wastaafu wengi kuwa na mikopo ya benki ambayo husababisha kufanyiwa makato makubwa kwenye pensheni zao, hivyo kupokea kiasi kidogo kuliko walivyotarajia.

Ameeleza kuwa hali hiyo huwafanya baadhi ya wanufaika waonekane kana kwamba mafao yao ni madogo, wakati chanzo kikuu ni mzigo wa mikopo.

Bw. Kadege amesema NSSF imejipanga kukabiliana na changamoto hizo kwa kuimarisha mafunzo ya maandalizi ya kustaafu, kutoa elimu ya fedha na kushauri wanachama kupanga vyema mikopo yao kabla ya kufikia umri wa kustaafu.

Amesisitiza kuwa lengo la mfuko huo ni kuhakikisha kila mwanachama anatumia mafao yake kwa njia itakayomuwezesha kuishi maisha bora, yenye utulivu na heshima uzeeni.      

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG