
NA JOHN ISRAEL, DODMA
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Khamis Mwinjuma, amesema kuwa Serikali imepunguza kwa kiwango kikubwa ada za leseni za huduma za maudhui mtandaoni kufikia 50,000 kwa mwaka, kufuatia maoni na ushauri uliotolewa na wadau mbalimbali wakiwemo vijana, wabunifu na wajasiriamali wanaotumia majukwaa ya kidijitali.
Ameyasema hayo Februari 12, 2026, wakati akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji unaofanyika katika Ukumbi wa New Generation jijini Dodoma.
Amesema kuwa gharama za leseni zilizokuwepo hapo awali zilikuwa kikwazo kwa wengi kurasimisha shughuli zao na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali, hatua iliyosababisha Serikali kutoa maelekezo kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufanya mapitio ya ada hizo. Aidha, amebainisha kuwa mapitio hayo yameleta nafuu kubwa kwa watoa maudhui mtandaoni.
Pia ameongeza kuwa ada ya leseni imepunguzwa kutoka Sh500,000 hadi Sh50,000, huku ada ya maombi ikiwa Sh10,000 pekee. Aidha, amesema kuwa kwa wakusanyaji wa maudhui mtandaoni, ada ya leseni imepunguzwa kutoka Sh1,000,000 hadi Sh100,000 na ada ya maombi ikiwa Sh20,000.
Amesema hatua hizo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kupunguza gharama za uendeshaji, kuhamasisha urasimishaji wa shughuli za kidijitali na kupanua fursa za ajira kwa vijana.
“Serikali inaamini kuwa kwa gharama hizi rafiki na jumuishi, wadau wengi zaidi wataingia katika mfumo rasmi,” amesema Naibu Waziri Mwinjuma.
Katika hatua nyingine, Mwinjuma amesema kuwa hadi kufikia Desemba 2025 jumla ya leseni 707 za utangazaji zilikuwa zimetolewa, akibainisha kuwa ukuaji huo unahitaji kuzingatia ubora wa maudhui na maadili ya taaluma. Aidha, amebainisha kuwa taratibu za kuanzisha utangazaji wa redio wa kidijitali zimekamilika ili kuongeza thamani katika sekta ya utangazaji.
Pia ameongeza kuwa wanahabari 2,454 wamepatiwa mafunzo katika kipindi cha mwaka uliopita, hatua iliyolenga kuimarisha uandishi wa habari za maendeleo. Hata hivyo, amesema kuwa mafunzo hayo yatazaa matunda endapo maslahi ya wanahabari yatapewa kipaumbele, akieleza kupokea malalamiko ya baadhi yao kufanya kazi bila mikataba na wengine kutolipwa kwa muda mrefu.
Aidha, amebainisha kuwa Wizara imeanza mazungumzo na taasisi mbalimbali za Serikali kupitia upya tozo zinazokwamisha ustawi wa vyombo vya habari, hususan vya vijijini, pamoja na kushughulikia madeni ya matangazo ya Serikali yanayodaiwa na vyombo vya habari.
