
NA DENIS MLOWE IRINGA
MAHAKAMA ya Tanzania imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kusimamia haki kwa uadilifu, weledi na bila kuogopa wala kupendelea upande wowote, ikibainisha kuwa utawala wa sheria ndio msingi thabiti wa amani, ustawi wa jamii na maendeleo endelevu ya taifa.
Akizungumza leo katika maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika kwenye viunga vya Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Jaji Mfawidhi Dunstan Ndunguru alisema Mahakama itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kikatiba kwa kuhakikisha haki inatolewa kwa wakati, kwa usawa na bila kuingiliwa na chombo chochote.
“Majaji na Mahakimu tumekabidhiwa jukumu kubwa la kusimamia haki. Tunapaswa kuwa wanyenyekevu mbele ya ukweli na kusimama imara bila kuyumbishwa. Tunasema bayana kwamba tutatenda haki bila hofu,” alisema Jaji Ndunguru.
Amefafanua kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaipa Mahakama uhuru kamili wa kusimamia na kutoa haki, huku ikielekeza haki kutolewa bila upendeleo na bila ucheleweshaji, jambo ambalo limeendelea kuongeza imani ya wananchi kwa mhimili huo muhimu wa dola.
Aidha, Jaji Ndunguru aliishukuru Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini na wadau mbalimbali wa utoaji haki kwa ushirikiano wao, akisema umekuwa mchango mkubwa katika kuimarisha utawala wa sheria na kupunguza migogoro katika jamii.
“Maendeleo ya kweli hayaanzi na miradi mikubwa pekee. Huanzia kwenye amani ya mioyo na uhakika wa haki kwa wananchi,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tanganyika Law Society (TLS) Kanda ya Iringa, Wakili Moses Ambindwile, alisema maadhimisho ya Siku ya Sheria ni tukio muhimu la kitaifa linalotoa mwanya wa kutafakari nafasi ya Mahakama katika mustakabali wa jamii na maendeleo ya nchi.
“Hatujadili sheria kama maandishi ya vitabuni pekee, bali mchango wa Mahakama katika uchumi, utulivu na ustawi wa taifa. Bila Mahakama thabiti, maendeleo hubaki kuwa ndoto,” alisema Ambindwile.
Naye Chivanenda Luwongo kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, aliahidi kuendeleza ushirikiano na Mahakama ili kuhakikisha misingi ya haki, uwajibikaji na utawala wa sheria inasimama imara kwa manufaa ya wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, aliipongeza Mahakama kwa kasi yake ya kusikiliza na kuamua mashauri bila kuchelewa, hatua ambayo imesaidia kupunguza migogoro na kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli za maendeleo.
“Jamii inayoiamini Mahakama ni jamii yenye amani, mshikamano na dira sahihi ya kimaendeleo,” alisema James.
Maadhimisho ya Siku ya Sheria huadhimishwa kila mwaka kama ishara ya kuanza kwa mwaka mpya wa Mahakama, yakileta pamoja wadau wa sekta ya sheria kujadili mafanikio, changamoto na mwelekeo wa mhimili huo katika kusimamia haki kwa manufaa ya taifa.

Tags
Mahakama