Na A/Insp Stephen Ngolongolo na Ssgt Mawazo Mtondo - Dodoma.
Mkuu wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Katungu, leo Februari 4, 2026, amefungua rasmi Mafunzo ya Utafiti kuhusu Ufanisi wa Programu za Urekebishaji wa Wafungwa. Mafunzo hayo yatadumu kwa siku tatu kuanzia Februari 4 hadi 6, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Rugimbana uliopo Msalato, Jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, CGP Katungu amesema kuwa katika kuimarisha huduma za urekebishaji, Jeshi la Magereza limefanya mapitio ya kina ya utaratibu wa awali na kuandaa mwongozo mpya wa urekebishaji wa wafungwa. Mwongozo huo umejikita katika hatua nne muhimu za urekebishaji, ikiwemo hatua ya mapokezi ya wafungwa.
Aidha, amesema Jeshi la Magereza limekuwa likishirikiana na taasisi mbalimbali, zikiwemo Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) pamoja na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), katika kutambua na kuendeleza ujuzi wa wafungwa wanaposhiriki katika shughuli mbalimbali za uzalishaji na mafunzo.
CGP Katungu ameongeza kuwa hivi karibuni Jeshi la Magereza, kwa kushirikiana na mamlaka zinazosimamia mitihani ya kitaifa, lilitoa fursa na kuandaa mazingira kwa mahabusu 12 waliokuwa wakishikiliwa katika Gereza la Babati kufanya Mitihani ya Kidato cha Nne mwaka 2025. Matokeo ya mitihani hiyo yalionesha kuwa mahabusu wanne (4) walipata ufaulu wa Daraja la Kwanza (Div I), mmoja (1) Daraja la Pili (Div II), watano (5) Daraja la Tatu (Div III) na wawili (2) Daraja la Nne (Div IV). Mafanikio hayo yameelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za Jeshi la Magereza katika kutoa elimu na mafunzo kama nguzo muhimu ya huduma za urekebishaji.
Kwa upande wake, Kamishna wa Fedha na Mipango wa Jeshi la Magereza, CP Chacha Binna Jackson, amesema kuwa utafiti ni nyenzo muhimu ya kitaaluma na kitaalamu katika kuboresha utendaji kazi. Ameahidi kuwa Jeshi la Magereza litaendelea kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) katika kuboresha na kuimarisha tafiti mbalimbali ndani ya Jeshi.
Naye, Mkuu wa Sehemu ya Utafiti Jeshi la Magereza, Naibu Kamishna wa Jeshi la Magereza, DCP Justine Kaziulaya, amewataka washiriki wa mafunzo hayo kusikiliza kwa makini mada zitakazowasilishwa na kuwa huru kuuliza maswali pale watakapohitaji ufafanuzi. Ameeleza kuwa mada zitakazofundishwa ni pamoja na majukumu ya Jeshi la Magereza na mtazamo wa ndani wa urekebishaji, maadili ya utafiti, mbinu za utafiti, ukusanyaji wa takwimu kwa malengo mbalimbali ya utafiti, utambuzi wa zana za utafiti zitakazotumika kujaza dodoso, pamoja na kufanya pre-test ya zana za utafiti katika magereza jirani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uratibu, Utafiti na Shughuli za Kitakwimu kutoka NBS, Dkt. Emiliana Karugendo, amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Jeshi la Magereza na NBS katika kushauriana na kubadilishana takwimu. Amesisitiza kuwa NBS iko tayari kutoa wataalamu kwa ajili ya kushirikiana na Jeshi la Magereza ili kupata takwimu sahihi na zenye ubora kwa matumizi ya kitaifa.
Tags
HABARI












