Tanzania na Uganda zinatarajiwa zinaendelea kuimarisha ushirikiano wao wa kimkakati , kufuatia ziara ya kikazi ya Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, anayetarajiwa kuwasili nchini 07/February/2026 kwa mazungumzo ya ngazi ya juu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Katika ziara hiyo, viongozi hao wawili wanatarajiwa kujadili kwa kina maendeleo ya Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP), mradi mkubwa wa kihistoria unaokaribia kukamilika na unaoendelea kuwa moja ya nguzo kuu ya ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia kati ya Tanzania na Uganda.
Mazungumzo ya viongozi hao yanatarajiwa kusisitiza dhamira ya pamoja ya kuhakikisha EACOP unakamilika kwa mafanikio, huku mradi huo ukiendelea kuiweka Tanzania katika nafasi ya kipekee kama kitovu cha nishati, miundombinu na uwekezaji Afrika Mashariki.
Kupitia EACOP, Tanzania inaendelea kunufaika kwa kuongeza mapato ya taifa, kufungua maelfu ya ajira kwa wananchi, kukuza uchumi wa mikoa inayopitiwa na bomba hilo na kuimarisha zaidi mahusiano ya kindugu na kihistoria na Uganda.
Ziara hii inayotarajiwa kufanyika pia inalenga kuimarisha ushirikiano katika maeneo mengine muhimu yakiwemo biashara, uwekezaji, miundombinu na usalama, hatua inayothibitisha uaminifu na mshikamano uliopo kati ya mataifa haya mawili.
