Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, amewataka viongozi wa upinzani Tundu Lissu na John Heche kujitokeza kwenye mdahalo wa wazi ili kujadili hoja za kisiasa.
Ametoa kauli hiyo leo Machi 7, 2026 wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Maswa, mkoani Simiyu
Kihongosi amesema chama chake kiko tayari kukutana nao mezani kwa ajili ya mdahalo wa hoja kwa hoja ili wananchi waweze kusikia na kutathmini hoja za pande zote.
"Mimi naongeaga ukweli, na wao nataka waje akae mmoja hapa, mwingine hapa kila mmoja aanze kupiga ukweli hapa, mimi nawatamani wale, kama ni Heche njoo kaa hapa, kama ni Tundu kaa hapa, halafu tujenge hoja tuone watafika wapi, hawatakuwa na hoja watapaniki." amesema Kihongosi
Amesema CCM inaamini katika kujibu hoja kwa kutumia takwimu na maelezo ya kina badala ya malumbano.
"Sisi CCM hatufoki, hatugombi tunawapa data, kwahiyo muwaambie waje tukae kwenye meza tuweke mdahalo halafu tuone hiyo battle" amesema