Ndugu wa raia wa Kenya, waliodanganywa kwenda kupigana katika safu ya jeshi la Urusi nchini Ukraine, waandamana Nairobi, Kenya, mnamo Machi 5, 2026. © Simon Maina / AFP
Na mwandishi wetu huko Nairobi, Albane Thirouard
Familia zao zina wasiwasi kuhusu hatima yao. Dazeni kadhaa kati yao waliandamana siku ya Alhamisi, Machi 5, katikati mwa jiji la Nairobi wameomba wapendwa wao warudishwe nyumbani haraka iwezekanavyo.
"Warudisheni watoto wetu": hivi ndivyo familia za Wakenya zisizo na habari za wapendwa wao nchini Urusi zinadai. Susan Kuloba alikuja na picha za mwanawe mkubwa, David. Aliahidiwa kazi kama mlinzi wa usalama, alisema. Aliishia kutumwa katika vita vya Urusi na Ukraine. Susan aliarifiwa na Mkenya mwingine kwamba mwanae aliuawa na droni. Aliwasiliana na mwanae kwa mara ya mwisho mwezi Oktoba mwaka uliyopita.
"Alinitumia picha hii. Unaweza kumuona akiwa amevaa sare yake ya kijeshi. Aliogopa, lakini angefanya nini? Aliniambia kwamba angekataa, kamanda angemuua mwenyewe. Leo, ninachotaka ni mwanangu arudishwe nyumbani. Ikiwa yuko hai, mrudisheni nyumbani. Ikiwa amefariki, rudisheni mwili wake nyumbani pia, ili niweze kupanga mazishi yake. Kusubiri bila kujua alipo ni jambo baya," anaelezea.
Ombi la kutaka hatua zaidi zichukuliwe kutoka kwa mamlaka
Janet Wainaina, kwa upande wake, alikuja kwa ajili ya kaka yake Samuel, ambaye anasema pia aliondoka nchini kwenda Urusi kwa kazi kama mlinzi wa usalama. "Tulienda kwenye ubalozi wa Urusi, ubalozi wa Ukraine, Wizara ya Masuala ya Diaspora, Wizara ya Mambo ya Nje ... Hakuna anayeweza kutupa majibu yoyote. Hatujapokea taarifa yoyote kuhusu kama yuko hai, yuko hospitalini, au amefariki ... Tunataka serikali yetu izungumze na serikali ya Urusi ili kupata majibu," amesema.
Waandamanaji waliwasilisha ombi kwa mamlaka wakitaka hatua zaidi zichukuliwe. Miongoni mwa madai yao: kurejeshwa kwa wapendwa wao na taarifa rasmi ya kupiga marufuku ya Wakenya kuajiriwa katika jeshi la Urusi.