Na Silivia Amandius.
Bukoba.
Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini,Mh. Johnston Mutasingwa, ameendelea kudhihirisha moyo wa kujali kwa wananchi wake baada ya kufikisha msaada kwa makundi maalum na wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Kata ya Kibeta, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono kipindi cha Mfungo wa Kwaresima na Ramadhani.
Msaada huo uliwasilishwa kwa niaba yake na Katibu wake, Ndugu Simba Leo march 18, 2026, ambaye alieleza kuwa licha ya Mbunge huyo kuwa nje ya jimbo kwa majukumu ya kitaifa, bado anaendelea kufuatilia kwa karibu hali za wananchi wake na kuhakikisha wanapata msaada unaohitajika.
Akizungumza wakati wa ugawaji wa msaada huo, Ndugu Simba alisema lengo ni kuwafikia wananchi walioko kwenye mazingira magumu, hususan wazee, watu wenye ulemavu pamoja na kaya zenye kipato cha chini zinazofaidika na mpango wa TASAF.
Wananchi waliopokea msaada huo walionesha furaha na shukrani zao, wakieleza kuwa msaada huo umekuja kwa wakati muafaka na umewapa faraja kubwa katika kipindi hiki cha mfungo.
Hatua hiyo imeendelea kuimarisha uhusiano kati ya viongozi na wananchi, huku ikiakisi dhamira ya kuhakikisha makundi yenye uhitaji yanapata msaada na kuimarishiwa ustawi wao wa maisha kila siku.

