
NA DENIS MLOWE, IRINGA
SHIRIKA la DSW kwa kushirikiana na TAHEA kupitia mradi unaolenga kujenga jamii imara, yenye uwezo, salama na inayostawi (REST) limeendesha mdahalo wa pamoja katika Kata ya Ifunda, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, uliolenga kutoa elimu kuhusu afya ya uzazi na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Mdahalo huo uliwakutanisha wadau mbalimbali wa jamii wakiwemo wazazi, viongozi wa serikali za mitaa pamoja na wanafunzi kwa lengo la kuongeza uelewa wa jamii kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia na namna ya kuuzuia.
Akizungumza wakati wa mdahalo huo, Afisa Mradi wa REST katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Hidaya Juma amesema kuwa mdahalo huo ni sehemu ya mwendelezo wa jitihada za kuwafikia wananchi katika kata mbalimbali ili kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya afya ya uzazi na haki za binadamu.
Amesema kupitia mradi huo, elimu inaendelea kutolewa katika maeneo tofauti ikiwemo kata za Ifunda, Tanangozi, Kihorogota na Kising’a ili kuhakikisha jamii inapata uelewa sahihi kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia.
Hidaya amesema lengo la mdahalo huo ni kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika kupinga vitendo vya ukatili na kutoa taarifa pindi wanapobaini matukio hayo katika jamii zao.
Akitoa elimu kwa washiriki wa mdahalo huo, Mtendaji wa Kata ya Ifunda, Happiness Mkongwa aliwataka wanaume kuacha kuficha matukio ya ukatili wanayokumbana nayo ndani ya familia na badala yake wajitokeze kuyatolea taarifa kwa vyombo husika.
Amesema mara nyingi wanaume wamekuwa wakinyamaza wanapokumbana na vitendo vya ukatili wa kijinsia jambo linalochangia kuendelea kwa vitendo hivyo bila kuchukuliwa hatua stahiki.
Kwa upande wake Afisa Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Hamis Sabuni amewahimiza vijana kuwa mabalozi wa kupinga ukatili wa kijinsia katika jamii zao.
Sabuni amesema vijana wanapaswa kuwa sehemu ya suluhisho kwa kuelimisha wenzao na kuripoti matukio ya ukatili badala ya kuyafumbia macho.
Aidha ametoa onyo kwa jamii kuacha tabia ya kuyasuluhisha matukio ya ukatili wa kijinsia ndani ya familia kwani kufanya hivyo kunawanyima haki wahanga na kuendelea kuchochea vitendo hivyo katika jamii.
