Nimeona mijadala kadhaa kuhusu "ASKOFU MWANAMKE" na hata baadhi ya wasomaji wangu wameniuliza maswali kadha. Wacha niseme machache, kisha tutawaza pamoja kibanangabananga na kisha salaam nitawasalimia.
Dini na Imani ni mambo mawili tofauti na hivyo "Dini za Kikristo" siyo "Ukristo", bali mapokeo (Uislamu unaita Hadithi) ambayo yametokana ama kujengwa kwenye misingi ya imani, mwenendo na fundisho la watangulizi katika imani. Ndiyo maana ndani ya kila DINI yako MADHEHEBU na ingawa yote msingi wake ni kitabu (falsafa) kimoja mfano Biblia au Quran. Inaweza ikakushangaza na baadhi ya "wafia Dini" (Mafarisayo na Masadukayo wa zama zetu) masikio yatawasha, lakini Ukristo wenyewe hasa ni imani siyo Dini hata Yesu (aitwaye Kristo) hakuwa, siyo na hatakuwa Mkristo. Yesu ndiye Kristo.
Kristo ni neno lililotoholewa kutoka Kiingereza Christ ambalo nalo lilitoholewa kutoka Kigiriki "Christos" likitafsiri neno la Kiebrania "Mashiach" ama Masihi kwa Kiswahili cha Nyerere na TANU, na neno hili lilitumiwa tangu kale kabla ya kuzaliwa Yesu aitwaye Kristo likinasibishwa na neno la Kiharamu "chrio", yaani "kupakwa" asomaye na afahamu!
Kupakwa. Hapo zamani katika Mila na Desturi za Uyahudi (ulio baba wa Ukristo, Uislamu, Rastafarian, Ubahai, na hata Ubabhi), walipakwa mafuta watu watatu, yaani Nabii, Kuhani, na Mfalme kwa majukumu tofauti, na kupakwa mafuta huko (Christening) kulimaanisha watu hao kutengwa kutoka kati ya wanadamu kwa jukumu ama wito maalumu wa kiungu kuhusu wanadamu ama jamii zao (Waebrania 5:1). Watatu hawa, yaani Nabii (muonaji mwenye jukumu la kusikia na kuona Maono ya Mungu na kuleta ujumbe huo kwa watu), Kuhani (Kiongozi wa ibada mwenye jukumu la kuongoza ibada ikiwamo utoaji wa sadaka na dhabihu akiingia "patakatifu pa patakatifu" kwa ajili yake mwenyewe ba ndugu zake), na Mfalme (Kiongozi wa Serikali na mtangulizi wa watu vitani), walipata mamlaka yao katika Torati iliyokuwa mfano wa Katiba katika jamii ya Kitheoklasia ya zama hizo. Ndiyo maana Daudi mwana wa Yese anakataa mara tatu kuunyosha mkono wake dhidi ya "Masihi" (Christos) wa Bwana, na hata Paulo Mtume anaomba radhi pale anapomtolewa maneno makali Anania baada ya Anania kuamuru anaswe kibao kinyume na sheria, kwa vile pamoja na upotofu huo, Anania alikuwa "Kuhani" Mkuu. Muda usingenitosha kuleta habari za Skewa "Kuhani Mkuu" na wanawe walipoamua kukemea Pepo kwa jina la Yesu na kuchaniwa nguo na kadhalika.
Askofu. Neno ama jina Askofu limetajwa mara Nne tu katika Biblia na zote hizi katika Agano jipya, na hiyo ingemaanisha kwamba jina ama nafasi ya Askofu ilianza kutumika rasmi katika Kanisa' kati ya miaka 50-70 baada ya Kristo. Naona sababu kadhaa, lakini mbili kubwa; kwanza kwamba Ukristo kama Dini ulianza baada ya Yesu kufufuka na kuondoka duniani, miaka takribani 70, na hivyo Yesu hakuacha duniani "mfumo" wa kidini ama dhehebu wa mafundisho yake, aliacha harakati zilizojengwa juu ya itikadi za Yesu Masihi, mwana yule wa Seremala kutoka Nazarethi, anayeaminika kufa na kufufuka kutoka kwa wafu, asomaye na afahamu! Hata hivyo, neno Askofu lilikuwako na lilitumika kwa miaka mingi kama cheo cha "kisiasa" au Utawala kumaanisha "msimamizi, mwangalizi, gavana, au tungeweza kusema Mkuu wa Mkoa". Lilitumika pia kwenye muktadha wa kijeshi kumaanisha Jenerali msimamizi wa kijeshi na hata linaaminika kutumika kwenye jamii mchanganyiko wa Kigiriki, Kihindi na Ulaya kumaanisha "Shushushu" au kwa kiloni "Spy" yaani "skopos" kwa Kigiriki.
Tungeweza kwenda mbali zaidi na kuchanganua mengi, lakini itoshe kusema, kwa mujibu wa imani ya Uyahudi ambao ndiyo Baba wa Ukristo, hakukuwa na hata sasa hakujakuwako na "Kuhani" Mwanamke, na majukumu ya Kuhani yalihusisha kupanda madhabahuni na kutoa dhabihu na hakujakuwako na mwanamke aliyetoa dhabihu katika Biblia hata sasa. Ni kweli kwamba kumekuwako na Manabii Wanawake na hata viongozi wa kisiasa na kijeshi Wanawake katika Biblia na historia, lakini hakujakuwako na Kuhani Mwanamke wakati wowote katika Biblia yote, na hivyo kwangu mimi kuwako kwa Kuhani Mkuu mwanamke ni ukengeufu kutoka katika Biblia na uasi tu wa kizazi chetu dhidi ya kanuni za kiungu katika kutafuta kuwako kwa "Haki" za binadamu bila wajibu wa binadamu kukaa katika mipaka yake. Hainishangazi hata hivyo, ikiwa hata Mashoga wamesimikwa katika nafasi za Ukuhani na hivyo kuwako Askofu mwanamke huenda siyo Kwa nafasi ya Ukuhani, bali Utawala wa kisiasa na hata Ushushushu "skopos" kwa sababu Dini siyo imani na Kanisa' siyo Dini, asomaye na afahamu, Mimi hizi ni salaam tu nawasalimia.
Wasalaam