BANDA MEDIA BLOG

OPERESHENI MBINGA DC: KASHUSHURA AANZA NA WALIMU WA HISABATI KUINUA TAALUMA

 


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma Joseph Kashshura Rwiza,akizungumza katika baraza la Madiwani ambapo alisisitiza kuhusu madiwani kushirikiana na watendaji wa vijiji na walimu katika kuinua kiwango cha taaluma mashuleni.

………….
Na Muhidin Amri, Mbinga
HALMASHAURI  ya Wilaya Mbinga Mkoa wa Ruvuma, imeweka mikakati ya  kuinua kiwango cha ufaulu na kuboresha ufundishaji, ujifunzaji na ufuatiliaji wa maendeleo ya wanafunzi katika shule za msingi na sekondari.
Miongoni  mwa  mikakati iliyowekwa ni pamoja na kufanya mitihani tembezi, kuendesha vikao vya walimu wa masomo, wakuu wa shule pamoja na maafisa elimu kata ili kujadili mbinu bora za kuboresha ufaulu wa wanafunzi.
Aidha Halmashauri hiyo imepanga kufanya tathmini ya kila mtihani ambayo itafanyika katika ngazi za shule, kata na Halmashauri ili kubaini changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi mapema pamoja na kuimarisha ufundishaji kuanzia elimu ya awali, shule za msingi hadi sekondari kwa kusimamia ukamilishaji wa mada zote za masomo kwa wakati.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Joseph Kashushura alisema hayo wakati akizungumza na walimu wote wa shule za msingi na sekondari wanaofundish amasomo ya Hesabu na ametaja mikakati mingine ni kufanya ukaguzi wa shule kwa wakati ili kubaini mapungufu na kuyafanyia kazi mapema, kuhimiza mahudhurio ya wanafunzi shuleni,na kuhakikisha wanafunzi wanapata msingi mzuri wa kusoma, kuandika na kuhesabu.
Alisema, kutakuwa na usimamizi  wa utoaji wa majaribio ya mara kwa mara ili kufuatilia maendeleo ya wanafunzi, kuimarisha klabu za masomo kwa walimu na wanafunzi, pamoja na kuhimiza matumizi ya teknolojia na vifaa vya kielektroniki katika ufundishaji na ujifunzaji.
Kashushura alisema,mikakati hiyo ni harakati za kuinua kiwango cha taaluma, hususani somo la Hisabati ambapo amekutana na walimu wa somo la hisabati toka shule za Msingi lengo likiwa ni kuweka mikakati ya kutokomeza ufaulu hafifu.
Kashushura amebainisha kuwa, lengo la kuwaita walimu wa Hisabati ni kufanya tathimini ya matokeo ya darasa la saba mwaka 2025 ambapo ufaulu wa wanafunzi hususani somo la Hisabati haukuwa mzuri.
” Ndugu zangu walimu,uchambuzi wa somo la Hisabati kwa Kata zote   29 katika Halmashauri yetu ni kama ifuatavyo; wanafunzi waliofanya mtihani wa somo la Hisabati walikuwa 5968,waliopata daraja  A ni 65 tu, waliopata daraja  B ni 397 Waliopata daraja  C ni 1712, waliopata daraja D  ni  2729, waliopata daraja E ni  wanafunzi 965. Kwa hali hii hatuwezi kunyamaza kabis ,nadhani mmeona hali halisi, sijawaita kwa nia mbaya, bali kwa ajili ya kujenga nataka tuwe na lengo moja ya kuinua taaluma yetu.” alisisitiza Kashushura.
Mkurugenzi Kashushura aliongeza kuwa, ameanza na shule za msingi, atafika hadi shule za sekondari ili kuhakikisha kuwa mnyororo mzima wa elimu unakuwa imara. Lengo kuu ni kuweka msingi madhubuti kuanzia ngazi za chini ili kufikia malengo ya kitaifa ya taaluma.
” Mbinga DC tunafanya vizuri sana kwenye maeneo mengine, hivyo lazima tuweke nguvu tufanye vizuri kwenye elimu,Wiki iliyopita tumetembelea shule za Msingi na Sekondari katika Kata tatu ambazo ni Linda, Mkumbi na Mkako. Tumekuta changamoto nyingi , mapungufu tumeyaainisha na hatua zimechukuliwa kwa walimu husika.” alisema Kashushura.
Kashushura,aliwasihi walimu kurudi madarasani wakafundishe wanafunzi waive vizuri, kwani  kuanzisha kambi ikiwa wanafunzi hawajafundishwa hawatapata matokeo mazuri.
na Serikali inatambua changamoto za mazingira ya kazi, na Serikali inaendelea kuzifanyia kazi,lakini kwa sasa, tuinue taaluma” alisisitiza Kashushura.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma Joseph Kashshura Rwiza,akizungumza katika baraza la Madiwani ambapo alisisitiza kuhusu madiwani kushirikiana na watendaji wa vijiji na walimu katika kuinua kiwango cha taaluma mashuleni.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG