
Na. Dennis Gondwe , Dodoma Jiji , IYUMBU
SHULE ya Sekondari Iyumbu ilipokea shilingi 158,000,000 kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa maabara tatu, vyumba viwili vya madarasa na jengo la utawala ikiwa ni juhudi za serikali za kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia shuleni hapo.
Akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi huo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Iyumbu, Mwl. Emanuela Luvyale alisema kuwa miradi hiyo ipo vizuri katika hatua za mwisho za umaliziaji. “Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara ulianza kwa nguvu za wananchi tangu mwaka 2020 ambapo wananchi walifanikiwa kujenga hadi hatua ya lenta. Mnamo tarehe 23/11/2025 Shule ya Sekondari Iyumbu ilipewa kiasi cha shilingi 128,000,000 kwa ajili ya kuendeleza mradi huu kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Shughuli zilizotarajiwa kufanyika ni kujenga upande mmoja ambao haukukamilika pamoja na kazi zote za ukamilishaji wa mradi kuanzia kumwaga lenta. Mpaka sasa mradi huu upo katika hatua ya kuweka mfumo wa gesi na bomba kwenye maabara ya Kemia na Baiolojia na kumimina meza kwa jengo la Fizikia” alisema Mwl. Luvyale.
Kuhusu ukamilishaji wa vyumba viwili vya madarasa alisema kuwa shule hiyo ilikuwa na upungufu wa vyumba hivyo kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2026. “Kupitia mapato ya ndani, halmashauri ilitoa kiasi cha shilingi 18,000,000 iliyoingizwa tarehe 23/11/2025, madarasa haya yalikuwa yamefikia hatua ya ‘blundering’. Kazi hizi zote za ukamilishaji wa madarasa zimefanyika kama ilivyopangwa na mradi huu umekamilika kwa asilimia 100. Ukamilishaji wa jengo la utawala, shule ilipokea kiasi cha shilingi 12,000,000 kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kukamilisha jengo la utawala ambalo lilikuwa halijakamilika kwa muda mrefu. Mradi huu ulihusisha kukamilisha jengo la utawala kwa kuchimba makaro mawili ya maji, kuweka ‘skatting’, kujenga makaro yote mawili, kumalizia kuweka ‘tiles’ nyuma ya jengo, kutengeneza ngazi rafiki, kupaka msingi wa jengo, kuingiza mfumo wa maji taka na safi na kurudia kupaka rangi jengo zima. Kazi zote zimekamilika” alisema Mwl. Luvyale.
Akiongea na wanafunzi, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Dodoma, Mohamed Jawadu alipongeza usimamizi na utekelezaji wa miradi hiyo na kusema kuwa wanafunzi wamebakiza wajibu wa kusoma kwa bidii. “Baada ya kuwa tumejiridhisha na yale CCM iliyoahidi yamefanyika, kwa kweli tunakushukuru sana Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kwa namna mlivyoendelea kushikiria mnyororo wa elimu chini ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwamba wanafunzi lazima wasome katika madarasa bora, madawatI mazuri, walimu wa kutosha na mkishakuwa na hivi vyote mtakuwa na uwezo wa kuwasilikiza walimu, kusoma vizuri na uwezo wa kuwa viongozi wa baadae” alisema Jawadu.Shule ya Sekondari Iyumbu ni shule iliyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi wa Kata ya Iyumbu mwaka 2019 ikiwa na wanafunzi 73 na walimu 07. Kwa sasa Shule ina jumla ya wanafunzi 403, wavulana 163 na wasichana 240, walimu wapo 30 kati ya hao wanaume 5 na wanawake 25.

