
Na Silivia Amandius.
Bukoba.
Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera imeendelea kuimarisha huduma ya umeme baada ya kukabidhi vitendea kazi vipya kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani humo vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja.
Vitendea kazi hivyo vinajumuisha magari, pikipiki pamoja na bajaji ambazo zitatumika kuwasaidia watumishi wa shirika hilo kuwafikia wananchi kwa haraka katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo na kushughulikia changamoto za umeme kwa wakati.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi na makabidhiano ya vifaa hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Ramadhani Yahya Kido amesema serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha miundombinu ya umeme ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo muhimu kwa ufanisi zaidi.
Amesema vitendea kazi hivyo vinapaswa kutumika ipasavyo na watumishi wa TANESCO ili kuongeza ufanisi wa kazi, kupunguza muda wa kushughulikia hitilafu za umeme pamoja na kuwafikia wananchi waliopo katika maeneo ya mbali kwa haraka.
Kanali Kido pia amewataka watumishi wa shirika hilo kufanya kazi kwa weledi, uwajibikaji na ushirikiano ili kuhakikisha malengo ya serikali ya kuwapatia wananchi huduma bora ya umeme yanafikiwa.
Kwa upande wake Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kagera Mhandisi Tawakal Seleman amesema shirika hilo linaendelea kupanua wigo wa huduma za umeme kwa wananchi huku likiwa na matarajio ya kuhudumia zaidi ya wateja laki 5 pamoja na kaya laki 315,000.kila mwaka.
Amesema kupatikana kwa vitendea kazi hivyo kutasaidia kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu ya shirika hilo, kurahisisha ufikaji katika maeneo mbalimbali pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Aidha ameishukuru serikali kwa kuendelea kuliwezesha shirika hilo kwa kuwapatia vitendea kazi vinavyorahisisha utendaji kazi wa watumishi na kusaidia kuifikisha huduma ya umeme kwa wananchi kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.
Mhandisi Seleman ameongeza kuwa TANESCO itaendelea kushirikiana na serikali pamoja na wananchi kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi wengi zaidi ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Mkoa wa Kagera
