
…………
Na Muhidin Amri, Mbinga
WAKALA wa Barabara za mijini na vijijini(TARURA)Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma,umepanga kutumia Sh.bilioni 2.5 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili kufanya matengenezo ya barabara zake huku vyanzo vikuu vya fedha hizo ni mfuko wa Jimbo,tozo na matengenezo ya barabara.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Tarura Wilayani Mbinga Mhandisi Oscar Mussa,wakati akiwasilisha mpango wa matengenezo na maboresho ya barabara kwenye kikao cha robo ya pili cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo eneo la Kihamili kata ya Kigonsera.
Aidha alisema,Tarura Wilaya ya Mbinga inasimia barabara zenye urefu wa kilometa 973.33 zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya Mbinga zilizopitiwa na kutangazwa na Gazeti la Serikali mwezi Juni 2021.
Alisema,katika Halmashauri hiyo kuna barabara 46 zinazojengwa zenye urefu wa kilometa 350 ambazo hazijatangwa kwenye gazeti la Serikali lakini kutokana na umuhimu wake Tarura inazihudumia ili kurahisisha usafiri,usafirishaji na kuchochea kukua kwa uchumi.
Alisema,bajeti ya mwaka 2026/2027 imezingatia zaidi miongozo ya serikali,miongozo na maagizo ya viongozi wa serikalia mabo mara kwa mara wamekuwa wakiwasilisha Tarura kwa ajili ya kuboresha maiundombinu ya barabara zilizopo.
Alisema,katika bajeti ya mwaka huu Tarura itafanya matengenezo ya barabara yenye urefu wa kilometa 74 ambazo zitachongwa,kuweka kifusi kilometa 32.6 na kujenga barabara ya lami wa mita 500 kutoka Barabara kuu ya Mbinga Songea kuelekea Hospitali ya Halmashauri ya wilaya iliyopo eneo maarufu la Hifadhi.
Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Kisare Makori,amempongeza Meneja wa Tarura Oscar Mussa kwa kazi nzuri ya kutekeleza ujenzi wa barabara ambazo zinapitika wakati wote wa mwaka na zina mchango mkubwa kiuchumi na maendeleo ya wananchi.
Diwani wa kata ya Amani makolo Ambrose Komba,ameipongeza Tarura kwa kuandaa bajeti nzuri inayokwenda kugusa moja kwa moja maisha ya wananchi hususani wanaoishi maeneo ya vijijini.
Amewasisitiza madiwani wenzake,kwenda kusimamia matumizi ya fedha hizo kwa kuboresha miundombinu ya barabara kwenye kata zao ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa hasa mazao kutoka shambani kupeleka sokoni.
“Bajeti hii ya Tarura imekaa vizuri sana,naiomba serikali itoa fedha hizo kwa wakati ili zitumike kwa malengo iliyokusudiwa,kuna baadhi ya maeneo katika Halmashauri yetu wananchi hasa wakati huu wa masika wanateseka sana kwa kukosa usafiri wa uhakika wanapotaka kutoka sehemu moja kwenda nyingine”alisema Komba.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Muungano Xveri Kayombo,ameipongeza Serikali kupitia Tarura kutenga zaidi ya Sh.bilioni 2 ambazo kama zitatolewa kwa wakati zitatua changamoto ya barabara katika Halmashauri ya Mbinga vijijini.
“Hizi fedha zikiletwa kwa wakati na namna meneja wetu wa Tarura na wasaidizi wake wanavyofanya kazi vizuri nina uhakika zitatatua changamoto kubwa ya barabara, barabara hizi zina umuhimu mkubwa kwani zinatoa huduma kwa wananchi hasa ikizingatia kuwa asilimia 100 ni wakulima”alisema Kayombo.