Dame Sarah Mullally wa Kanisa Anglikana
Mullally, anatarajiwa kusimikwa rasmi kama askofu wa Cantebury baadae mwezi huu, na uteuzi wake kama mwanamke wa Kwanza kuongoza kanisa hilo Duniani, uliibua hisia mseto, hasa kutoka kwa waumini wa kikristo wenye msimamo wa kihafidhina ambao wanapinga wanawake kuhudumu kama maaskofu.
Kongamano la siku nne la mjini Abuja, limeandaliwa na vuguvugu linalofahamika kama GAFCON, ambapo liliundwa mwaka 2008 kufuatia tofauti za kitheolojia, ikiwemo kuhusu ufungishaji wa ndoa za watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
Vuguvugu hili kwa sehemu kubwa limevutia wachungaji na waumini wengi waliogawanyika kutoka barani Afrika, ambapo baadhi wanaunga mkono uteuzi wa Mullally.
Muungano huu wa maaskofu kutoka Afrika, umekuwa katika mvutano hata na mtangulizi wa Mullally, askofu Justin Welby, ambaye alikuwa anaunga mkono ndoa za mashoga.
Ushirika wa Anglikana, dhehebu la tatu la kikristo kwa ukubwa duniani baada ya kanisa Katoliki na Orthodox ya Mashariki, linaundwa na majimbo 42 katika nchi 165, viongozi wake wakisema wanabaki kuwa familia ya makanisa yanayojitegemea lakini yanayotegemeana, licha ya kuongezeka kwa mvutano kuhusu theolojia na utawala.